January 7, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Nchi sita zapinga kukamatwa kwa Rais wa Venezuela

Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro

IKIWA ni siku moja imepita tangu vikosi vya Marekani kumkamata Rais Nicolas Maduro, Nchi sita ikiwemo Colombia zatoa taarifa ya pamoja zikitaja shambulio la Marekani dhidi ya Venezuela kuwa “mfano hatari.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Serikali za nchi sita ambazo ni pamoja na Colombia, Brazili, Chile, Mexico, Uruguay na Hispania zimetoa taarifa ya pamoja kuhusu hali nchini Venezuela, zikisema kwamba operesheni ya kijeshi ya upande mmoja dhidi ya Venezuela imeweka “mfano hatari sana” kwa amani na usalama wa kikanda.

Nchi hizo sita zimekuwa na wasiwasi mkubwa na kupinga hatua hiyo na kwamba zimetoa wito wa kutatua msukosuko huo kwa njia ya mazungumzo na majadiliano.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Colombia, nchi hizo sita zinaamini kwamba operesheni hiyo ya kijeshi imekiuka sheria ya kimataifa na kanuni za msingi za Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Zimesema hali nchini Venezuela lazima ishughulikiwe kwa amani na kwa kuongozwa na watu wa Venezuela, ambapo mchakato huo unapaswa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria ya kimataifa na bila kuingiliwa na nje.

Taarifa hiyo inasisitiza asili ya Amerika Kusini na Caribean kama eneo la amani, ikizitaka nchi za kikanda kuweka kando tofauti za kisiasa na kuungana ili kukabiliana kwa pamoja na vitendo vyovyote vinavyotishia utulivu wa kikanda.

Pia inamsihi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mifumo husika ya pande nyingi kuchukua jukumu la upatanishi na kutoa mchango kwa ajili ya kupunguza mvutano na kudumisha amani ya kikanda.

Marekani ilifanya operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya Venezuela mapema 3 Januari 2025 ikishambulia mji mkuu wa Venezuela, Caracas, na maeneo mengine, na kuwadhibiti kwa nguvu rais wa Venezuela Nicolás Maduro na mkewe, na kuwapeleka Marekani

About The Author

error: Content is protected !!