Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro
RAIS wa Venezuela, Nicolás Maduro, amekamatwa na kung’olewa mamlakani na Marakani, kufuatia mashambulizi makubwa nchini mwake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Waziri wa Ulinzi wa taifa hilo, Vladimir Padrino López, alitangaza kwamba vikosi vya kijeshi vya nchi hiyo vimesambazwa katika maeneo yote ya nchi, ili kukabiliana na waliyomuita, “adui wa taifa.”
“Wametushambulia, lakini hawatatutawala,” alisema waziri huyo wa ulinzi, huku akisisitiza kuwa Venezuela itapinga uwepo wowote wa majeshi ya kigeni katika ardhi yake.
Katika hotuba yake, Padrino López, alitoa wito wa mshikamano wa kitaifa mbele ya kile alichokiita “uvamizi mbaya zaidi kuwahi kufanywa dhidi ya Venezuela.”
Alisema, jeshi linafuata maelekezo ya Rais Maduro ya kuhamasisha vikosi vyote vya ulinzi.
Kupatikana kwa taarifa kuwa Marekani imefanya mashambulizi yaliyolenga maeneo ya kijeshi mjini Caracas na sehemu nyingine za nchi hiyo, kumekuja baada ya wiki kadhaa za shinikizo na malalamiko ya utawala wa Donald Trump dhidi ya Maduro.
Trump amekuwa akidai kuwa rais wa Venezuela hakushinda uchaguzi na anahusika katika biashara ya madawa ya kulevya na uhalifu unaohusiana na kuingiza dawa hizo nchini mwake.
Kwa mujibu wa maelezo yake, kwenye mtandao wa Truth Social, Trump amesema, Marekani imemkamata Maduro, pamoja na mke wake, baada ya mashambulizi makubwa ya kijeshi, ili kulinda usalama wake.

“Marekani imefanikiwa kutekeleza mashambulizi makubwa dhidi ya Venezuela na kiongozi wake, Rais Nicolás Maduro, ambaye yeye pamoja na mke wake wamekamatwa na kusafirishwa nje ya nchi,” alifafanua.
Trump aliongeza kuwa operesheni hiyo ilifanyika kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya Marekani, akisema maelezo zaidi yatatolewa baadaye.
Maafisa wameiambia CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, wameeleza kuwa Maduro, amekamatwa na kikosi cha Delta Force cha jeshi la Marekani.
Delta Force ni kikosi cha juu kabisa cha jeshi la Marekani kinachojihusisha na operesheni za kupambana na ugaidi.
Mapema Maduro alitangaza hali ya dharura katika eneo lote la taifa lake, kufuatia mashambulizi ya Jumamosi yaliyofanywa na Marekani.
Taarifa ya serikali ilisema, hatua ya serikali yake, “inalenga kulinda uhuru wa kisiasa na rasilimali za taifa.”
Aliagiza jeshi lake la taifa, kutekeleza mipango yote ya ulinzi “kwa wakati unaofaa na katika hali zinazofaa,” huku akihimiza vyombo vyote vya kijamii na kisiasa kushiriki katika kuhamasisha wananchi kudai mashambulizi hayo ni ya kikoloni.
Alisema, mashambulizi ya Marekani yamelenga “kubeba rasilimali za kimkakati, hasa mafuta na madini” na kuharibu uhuru wa kisiasa wa Venezuela.
ZINAZOFANANA
Chadema: Muda wa zuio la kufanya shughuli za siasa umekwisha
Kesi ya Mwambe yapigwa kalenda, kusikilizwa Januari 26
Tundu Lissu asherehekea Birthday gerezani