Mwenyekiti ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman
MWENYEKITI wa Taifa wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amewataka Watanzania kuutumia mwaka mpya wa 2026 kama fursa ya kuliponya Taifa na kulirejesha kwenye misingi sahihi ya kikatiba, kisheria na kimaadili, huku akisisitiza kuwa Taifa haliwezi kujengwa juu ya mifumo inayowanyima wananchi haki yao ya msingi ya kuamua uongozi wao. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Katika salamu zake za Mwaka Mpya zilizotolewa 1 Januari 2026, Masoud alisema pamoja na majaribu, mitihani na maafa yaliyotokea mwaka 2025, Taifa limeendelea kusimama jambo linalotoa nafasi ya kutafakari kwa kina mustakabali wa nchi na kuchukua maamuzi sahihi kwa maslahi ya wananchi wote.
Alipongeza Watanzania waliotoa mchango wao katika kurejesha utulivu nchini, huku akibainisha kuwa utulivu pekee haupaswi kuchukuliwa kama ishara ya amani ya kweli, bali kama fursa ya kujenga maridhiano ya kitaifa kwa misingi ya haki, ukweli na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi.
Masoud pia aliwapongeza watu waliothubutu kupaza sauti kupinga ufisadi, ukiukwaji wa Katiba, sheria na maadili, akisema vitendo hivyo vimesababisha maafa kwa Taifa, kupoteza uhai wa watu, mali za raia na kuichafua taswira ya Tanzania kimataifa, hata kwa mataifa rafiki wa jadi.
Akirejea misingi ya Katiba, alisisitiza kuwa mamlaka ya kuamua nani aongoze nchi yapo mikononi mwa wananchi kama inavyoelezwa katika Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara ya 9 ya Katiba ya Zanzibar, akionya kuwa sheria au maamuzi yoyote ya kiutawala yanayokwamisha haki hiyo ndiyo chanzo kikuu cha migogoro na kukosekana kwa amani ya kudumu.
Kuhusu Zanzibar, Masoud alisema kutokuwepo kwa mauaji wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 kulitokana na busara ya wananchi wa Zanzibar kuvuta subira, licha ya madai ya vitendo vya wizi na udanganyifu wa kura, akibainisha kuwa hatua za kisheria zilizochukuliwa na ACT Wazalendo zinalenga kutafuta suluhisho la kudumu kwa njia ya amani.
Alifafanua kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa haikuanzishwa ili kuhalalisha wizi wa uchaguzi, bali kuwa jukwaa la kujenga umoja, amani na maridhiano ya kweli, akisisitiza kuwa lengo la ACT Wazalendo si ushindi wa chama bali ni ushindi wa Zanzibar na Wazanzibari wote.
ZINAZOFANANA
Chadema: Muda wa zuio la kufanya shughuli za siasa umekwisha
Kesi ya Mwambe yapigwa kalenda, kusikilizwa Januari 26
Tundu Lissu asherehekea Birthday gerezani