SHEREHE za kuukaribisha mwaka mpya tayari zimeanza katika baadhi ya maeneo ya ulimwenguni, huku mataifa ya Pasifiki yakiongoza kuingia mwaka 2026 kabla ya sehemu nyingine za dunia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Miji na visiwa kadhaa tayari vimebadilisha kalenda, vimeingia mwaka 2026, huku mamilioni ya watu wakishuhudia fataki, sherehe za kitamaduni na mikusanyiko ya kifamilia kuashiria mwanzo wa mwaka mpya.
Jiji la Sydney nchini Australia, lilikuwa miongoni mwa maeneo ya kwanza yenye watu wengi kuukaribisha mwaka mpya kwa onyesho kubwa la fataki lililopamba anga la Bandari ya Sydney.
Mamia ya maelfu ya watu walikusanyika kushuhudia tukio hilo, ingawa furaha ilichanganyika na huzuni, baada ya tukio la shambulio lililotokea Bondi Beach mapema mwezi huu, lililoacha majonzi kwa wakazi wa jiji hilo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, sherehe pia zimeripotiwa katika mataifa jirani ya Pasifiki ikiwemo Fiji, Tonga na Samoa.
Wakaazi wa mataifa hayo, wamekusanyika kwa sala, ngoma za kitamaduni na fataki ndogo ndogo.
Wakati huohuo, Kisiwa cha Chatham cha New Zealand, kilicho mbali na bara hilo, kiliingia mwaka 2026 dakika 15 tu baada ya Kiritimati, kikifuata ratiba yake maalum ya muda.
Kwa upande wa kipekee, mfamasia mmoja kutoka Uingereza tayari ameukaribisha mwaka mpya akiwa Samoa, kabla ya kusafiri kwenda American Samoa, eneo ambalo lina saa tofauti, ili kuukaribisha tena mwaka mpya mara ya pilli, kitendo anachokielezea kama “kusafiri kwenye muda.”
Kadri saa zinavyoendelea kusogea, mataifa mengine duniani yakikiwemo ya Asia, Afrika, Ulaya na hatimaye Amerika yanajiandaa kuukaribisha mwaka mpya kwa matumaini mapya, sherehe na tafakari ya safari ya mwaka uliopita.
ZINAZOFANANA
Meridianbet yaleta mwanga wa mwisho wa Mwaka kwa akina kama Palestina hospitali
Matukio 5 yakukumbukwa na kutikisa zaidi 2025
Taifa Stars yafuzu 16 Bora AFCON