LINALOITWA Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limepata pigo la kufunga mwaka, baada ya Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, kuiondoa takwa la ulazima la kulitambua baraza hilo, kuwa jumuya ya Waislamu wote nchini. Anaripori Faki Sosi, Dar es Salaam … ( endelea).
Uamuzi huo umetolewa leo tarehe 24 Desemba 2025, na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, wakiongozwa na Jaji Elizabeth Mkwizu.
Majaji wengine, waliosikiliza shauri lilipopinga Bakwata kuwakilisha Waislamu wote nchini, walikuwa ni Jaji Awamu Mbagwa na Hamidu Mwanga.
Kesi ilifunguliwa na Sheikh Ayoub Salim Muinge, Sheikh Prof. Hamza Mustafa Njozi, Sheikh Ponda Issa Ponda, Bi. Riziki Shahari Ngwali na wenzao wengine tisa, wakiwamo wanazouni na walimu wa madrasa.
Mahakama imesema, Bakwata siyo taasisi inayobeba Waislamu wote nchini na kwa hivyo, taasisi za Kiislamu zinazotaka kusajiliwa au kupata huduma katika ofisi ya Msajili wa Jumuiya na Kabidhi Wasihi Mkuu wa Serikali, hazina wajibu wa kupitia BAKWATA ili kutimiza malengo yao.

Wadai walitaka Mahakama Kuu, kuamuru kwamba kitendo cha Msajili wa Jumuiya na Kabidhi Wasihi Mkuu kuwalazimisha Waislamu kuwa na barua inayowatambulisha kutoka Bakwata, ni kinyume cha sheria na Katiba, hoja ambayo imekubaliwa na mahakama.
Katika uamuzi wake, majaji wa Mahakama Kuu wamesema, Bakwata siyo baraza la waislamu wote kwa kuwa Uislamu una madhehebu mengine kama vile Shia.
“Ibara ya 8 ya Katiba ya Bakwata, inawataka viongozi wa baraza hilo kufuata madhehebu ya Suna Wal-Jamaa ya Imamu Shafii ikiwa kuna madhebu mengine yenye kufuata madhehebu tofuati na hayo,” alieleza Jaji Mkwizu kwa niaba ya wenzake.

The National Muslim Council of Tanzania (BAKWATA), liliundwa tarehe 17 Desemba 1968, baada ya serikali kuweka mkono, ili Waislamu wajiondoe kutoka kwenye taasisi ya East African Muslim Welfare Society, iliyokuwa ikiwaunganisha Waislamu wa Kenya, Tanzania na Uganda.
East African Muslim Welfare Society, ilikuwa moja ya taasisi zenye nguvu na ushawishi mkubwa nchini.
Taarifa zinasema, Bakwata ilianzishwa ili kuleta mshikamano kwa Waislamu na uislam, lakini sasa inatuhumiwa kujigeuza kuwa chombo cha serikali, jambo linalosababisha kupata upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya waislamu wenzao.
ZINAZOFANANA
Watumishi TEMESA wafutwe kazi – Mwigulu
2025, mwaka mchungu usiosahaulika
Jeshi la Polisi ni mwendo wa ‘kukanusha’