Mrajis wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Valentine Katema
MAJALADA 17 yanayohusu mashauri ya kupinga matokeo ya uchaguzi ya uwakilishi upande wa Unguja sasa yanamsubiri Jaji Mkuu wa Zanzibar ambaye ndiye wa kuyapangia majaji wa kuzisikiliza kesi mahkamani. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Hatua hiyo imefikiwa leo baada ya Mrajis wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Valentine Katema, kutamka rasmi kuwa hatua za awali za ufunguaji wa kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita zimekamilika.
Akieleza mbele ya wagombea waliofungua kesi kupigania haki ya ushindi katika uchaguzi uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025, kwenye kikao cha Mahkama Kuu ya Zanzibar iliopo Tunguu nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Mrajis Katema alisema kanuni za uendeshaji kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi zinaelekeza kuwa majalada yakishathibitishwa kuwa taratibu za awali zimekamilika inavyotakiwa, hufikishwa kwa Jaji Mkuu ambaye ndo mwenye jukumu la kuteua majaji wa kusikiliza kesi.
“Kwa kuwa mahkama hii imeridhika taratibu zote muhimu za ufunguaji wa mashauri haya zimekamilika kwa mujibu wa kanuni, ninayatuma majalada yote kwa Jaji Mkuu kwa ajili ya hatua inayofuata,” alisema Mrajis Katema akiakhirisha kikao kilichovutia makumi ya wanachama wa ACT Wazalendo wakiwemo viongozi wa kitaifa wa chama hicho pamoja na wagombea waliofungua kesi.
Kesi 17 zimewasilishwa mahakamani wagombea uwakilishi wakilalamikia matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar {ZEC} kupitia wasimamizi wake wa majimboni.
Leo, wakati taratibu za ufunguaji mashauri zikithibitishwa kukamilika, Wakili Suleiman Abdalla, ambaye pamoja na wakili Rajab Abdalla Rajab wanawakilisha jopo la wanaowatetea walalamikaji, aliomba hati za majibu ya majibu waliyowasilisha mahkamani kama walivyoahidi wiki iliyopita tarehe 10 Disemba kesi zilipotajwa kwa mara ya kwanza, wapatiwe mawakili wa walalamikiwa.
Walalamikiwa katika kesi hizo ni Wasimamizi wa Uchaguzi walioajiriwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Jopo la mawakili wanaowakilisha ni wanasheria waandamizi Salim Said, Mbarouk Suleiman Othman, Ali Issa Abdalla na Maulid Ame Mohamed anayeiwakilisha Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Majimbo husika ni Nungwi, Kijini, Mkwajuni, Chaani, Tumbatu, Bumbwini, Mtoni, Mwera, Welezo, Mwanakwerekwe, Pangawe, Kiembesamaki, Amani, Chumbuni, Mpendae, Malindi na Makunduchi.
Kesi nyengine nane zimefunguliwa kisiwani Pemba ambako zitatajwa tarehe 23 Disemba 2025 kufuatilia ukamilishaji wa taratibu za awali. Majimbo husika ni Kojani, Micheweni, Wawi, Chake Chake, Chonga, Kiwani, Chambani na Mkoani.
ZINAZOFANANA
Njama za kumlipa Singasinga zafichuka
KESI YA UNUNGE Z”BAR. Wakili aibana Serikali
Mwelekeo wa Chaumma ni upi?