Mkurugenzi Mtendaji wa EABL, Jane Karuku
KAMPUNI ya East African Breweries PLC (EABL) imetangaza kuwa kampuni ya Diageo imekubali kuuza hisa zake zote za EABL na umiliki wake katika kampuni ya vinywaji vikali ya UDV (Kenya) Limited kwa kampuni ya Asahi Group kutoka Japan. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hatua hii inaifanya Asahi kuwa kampuni ya kwanza kubwa kutoka Japan kuingia rasmi na kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika biashara ya vinywaji barani Afrika.
Baada ya ununuzi huu kukamilika, Asahi itakuwa mmiliki mkuu wa EABL na itasimamia shughuli zake zote nchini Kenya, Uganda na Tanzania. Kampuni hiyo imeeleza kuwa itaendelea kuziendeleza chapa za ndani ambazo wananchi wamezizoea, huku pia ikileta baadhi ya chapa zake maarufu duniani kwa walaji wa Afrika Mashariki.
Kwa makubaliano haya, Diageo inatarajia kupata mapato ya takribani dola bilioni 2.3 za Marekani baada ya kodi na gharama nyingine, sawa na shilingi Trilioni 5.69 za Tanzania. Thamani ya jumla ya EABL kwa makubaliano haya imekadiriwa kufikia dola bilioni 4.8, sawa na takribani Sh. 11.87 trilioni.
Ununuzi huu unaonesha imani kubwa ya wawekezaji katika ukuaji wa EABL na mustakabali wa soko la Afrika Mashariki, eneo ambalo linaendelea kukua kwa kasi kiuchumi na kwa idadi ya watu. Chini ya umiliki mpya, EABL inatarajiwa kuendelea kufanya vizuri na kupanua biashara yake zaidi.
EABL imeeleza kuwa inaingia katika ukurasa mpya wa ukuaji pamoja na Asahi, kampuni ambayo itanufaika na viwanda vya kisasa vya EABL, uzoefu wa uongozi wake, chapa imara, mtandao mzuri wa usambazaji pamoja na mahusiano mazuri na wafanyakazi, washirika na wateja.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa EABL, Jane Karuku, alisema kuwa ununuzi huo ni fursa kubwa kwa kampuni. Alisema mmiliki mpya analeta uzoefu mkubwa wa kimataifa katika ubunifu na ukuzaji wa chapa, jambo litakalosaidia EABL kufikia lengo lake la kuwa kampuni ya vinywaji inayoheshimika zaidi barani Afrika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa mpito wa Diageo, Nik Jhangiani, alisema Diageo inajivunia safari na mafanikio ya EABL katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania. Aliongeza kuwa Diageo itaendelea kushirikiana na Asahi kupitia matumizi ya baadhi ya chapa zake katika eneo la Afrika Mashariki, huku muamala huu ukiisaidia Diageo kuimarisha hali yake ya kifedha.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Asahi Group, Atsushi Katsuki, alisema EABL ni kampuni imara yenye nafasi kubwa sokoni, ikiwa na chapa zenye nguvu, viwanda vya kisasa na timu yenye uzoefu. Alisema Asahi inalenga kukuza biashara kwa njia endelevu na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi zinazohusika.
Muamala huu bado unahitaji kibali kutoka kwa mamlaka za serikali na unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka 2026. EABL imesisitiza kuwa hakutakuwa na mabadiliko katika shughuli zake za kila siku na hakuna wafanyakazi watakaopoteza ajira kutokana na mabadiliko haya.
Katika kipindi cha mpito, Diageo itaendelea kushirikiana na Asahi ili kuhakikisha mabadiliko yanafanyika kwa utulivu na shughuli zinaendelea bila usumbufu.
ZINAZOFANANA
Cheza michezo ya Wazdan, ondoka na kitita cha Mystery Multiplier
Tvbet ndani ya Meridianbet na uzoefu wa michezo ya kweli kwa wachezaji wa leo
Zawadi kukumwagikia kila mzunguko na Meridianbet Holiday Drops