November 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Zitto Kabwe azinduka usingizini

Zitto Kabwe

KIONGOZI mwandamizi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, sasa ametoka kwenye usingizi mnono. Amekiri kwamba hakuna uwezekano wa kulinda kura, kupitia chaguzi zinazofanywa kwa sheria kandamizi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akiandika kupitia ukurasa wake wa X zamani twitter, Zitto anasema, chama chake kilijaribu kulinda kura, lakini kimeshindwa.

“Kura hata kuhesabiwa hazikuhesabiwa. Zilitangazwa tu. Tulijaribu kulinda kura, tukashindwa,” anaeleza.

Kauli ya Zitto – mmoja wa viongozi wakuu wa ACT-Wazalendo – kwamba wameshindwa kulinda kura kwenye uchaguzi mkuu uliyopita, ni ya kwanza kutolewa hadharani, tangu kumalizika kwa uchaguzi huo.

Chama cha ACT-Wazalendo, kilitangaza kushiriki uchaguzi huo, kikiamini kuwa kinaweza kulinda kura na kukabiliana na ubakaji wa uchaguzi.

Kupitia kauli mbiu ya kulinda demokrasia, chama hicho kilisema, “Oktoba tutalinda kura. Hii ndio njia ya kulinda demokrasia.”

Lakini sasa, Zitto aliyejitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo la Kigoma Mjini na kuambulia kapa anasema, “…tumejaribu kulinda kura, tukashindwa. Tumekiri. Ni muhimu tuungane pamoja kupigania haki za watu.”

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kiliomba vyama vingine vya upinzani, kususia uchaguzi huo, badala yake, kuunganisha nguvu kutafuta mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi.

Uchaguzi wa 29 Oktoba, ambao ulimtangaza Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa mshindi wa asimia 98, katika maeneo mengi ya nchi, ulitawaliwa na vurugu zilizotokana na maandamano ya vijana maarufu kama Gen Z.

Maandamano hayo yalisababisha Tanzania kukumbwa na ghasia kubwa kwa siku tatu kuanzia siku ya uchaguzi (29 Oktoba), yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa na uharibifu wa mali za umma na binafsi.

Maandamano hayo ni makubwa kuliko yale ya Zanzibar ya tarehe 26 na 27 Januari 2001, Tanzania Visiwani, ambapo watu kadhaa waliuawa wakati wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), walipopinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, matukio ya 29 Oktoba mwaka huu, yameiweka serikali ya Rais Samia, katika nyakati ngumu zilizotikisa historia ya kisiasa ya nchini mwake.

Akizungumza baada ya kuapisha mawaziri wake wapya, tarehe 18 Novemba mwaka huu, mjini Dodoma, Rais Samia alikiri kuwa kilichotokea 29 Oktoba, kimechafua taswira ya nchi yake kimataifa.

About The Author

error: Content is protected !!