November 19, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Tume ya Rais Samia yapingwa kila kona

John Heche, Makamu wa Mwenyekiti wa Chadema

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema Tume ya Uchunguzi, iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, haina uhalali wa kufanya kazi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Jumatano, tarehe 19 Novemba 2025, makamu mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, ameeleza kuwa Rais Samia “hana uhalali wa kisiasa, kisheria na kimaadili wa kuunda chombo cha kuchunguza uhalifu uliotendeka.”

“Hii siyo tume huru ya uchunguzi. Hizi ni njama ya za kutaka kuficha ukweli, kufuta ushahidi na kuendelea kuwaumiza waathirika,” ameeleza kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini.

Amesema, chama chake, hakiitambui tume ya uchunguzi iliyoteuliwa na Rais Samia na kuitaka jumuiya ya kimataifa, kuingilia kati suala hilo kwa kuunda tume za uchunguzi.

Kauli ya Chadema imetolewa siku moja, baada ya Rais Samia kutangaza majina ya watu wanane, wanaounda kinachoitwa, “Tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba.”

Tume hiyo, inaongozwa na na Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Othman Chande na mrithi wake, Prof. Ibrahim Juma.

Wajumbe wengine, ni Balozi Ombeni Sefue, Katibu mkuu Kiongozi mstaafu; Balozi Radhia Msuya, Luteni Jenerali Paul Meela na Said Mwema, mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu-IJP.

Wengine, ni Balozi David Kapya, Dk. Stergomena Tax, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wakati wa maandamano.

Kwa mujibu wa Chadema, Samia ni Rais aliyejisimika madarakani bila ridhaa ya wananchi.

“Amejipachika urais kupitia mchakato usio huru, usio wa haki, usio wazi na usiokidhi viwango vya kidemokrasia kama ambavyo wameeleza waangalizi wa uchaguzi huo, kutoka Umoja wa Afrika (UA) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),” amefafanua.

Ameongeza, “Rais Samia hana mamlaka ya kimaadili wala kisiasa kuunda chombo cha kuchunguza uhalifu mkubwa uliofanywa na utawala wake dhidi ya raia waliokuwa wakidai haki zao za kidemokrasia na kikatiba.

“Kinachoitwa ‘kuchunguza uvunjifu wa amani’ ni mbinu ya kuwageuza waathirika kuwa wahalifu na kuwasafisha wahalifu halisi.”

Amesema, “…lengo ni kuendeleza ukandamizaji wa sauti huru na kuhalalisha utawala wa mabavu unaotekelezwa na serikali isiyo na ridhaa ya wananchi.”

Heche anasema, “kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi (Commissions of Inquiry Act, 2002, Chapter 32), tume ya aina hii ni chombo cha Rais, kinachofanya kazi kwa matakwa na maelekezo yake.”

Anasema, hata ripoti ya Tume, Rais ana mamlaka ya kuamua ichapishwe au isichapishwe, iwasilishwe hadharani au ifichwe.

Kwa mantiki hiyo, Heche anasema, “hiki siyo chombo huru, na hakiwezi kutoa ukweli wala haki katika mazingira ambapo serikali ndiyo mtuhumiwa mkuu.”

Anasema, wote walioteuliwa ndani ya tume hiyo, waliwahi kuwa au ni watumishi wa serikali na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), jambo ambalo kimsingi, linakiuka kanuni ya kimsingi kwamba tume huru haipaswi kuwa na uhusiano wowote na serikali wala chama tawala.

Heche anasema, Tume inayohitajika ni ya kuchunguza mauaji na siyo uvunjifu wa amani, na kwamba “haiwezekani mtuhumiwa akajichunguza mwenyewe halafu tutarajie haki.”

Tanzania ilikumbwa na ghasia za maandamano ya siku tatu kuanzia 29 Oktoba 2025, siku ya uchaguzi, yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa na uharibifu wa mali za umma na binafsi.

Maandamano hayo yanaelezwa ni makubwa kuliko yale ya Zanzibar ya 26 na 27 Januari 2001, Unguja na Pemba, ambapo watu kadhaa waliuawa wakati wafuasi wa upinzani walipopinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.

Katika hatua nyingine, Chama cha Wananchi (CUF), nacho kimepinga kuundwa kwa tume hiyo, kikisisitiza kuwa kwa yaliyotendeka nchini, kunahitajika chombo huru cha uchunguzi.

Chama cha Wananchi kinasema, kilikuwa chama cha kwanza na taasisi ya kwanza nchini kutoka hadharani, tarehe 5 Novemba 2025, kuzitaka Jumuiya za Kimataifa na za Kikanda kushiniza kufanyika kwa uchunguzi huru wa mauaji, uvunjaji wa haki za binadamu, uharibifu wa mali na uhalifu wa uchaguzi.

“CUF – Chama cha Wananchi – bado kinasisitiza umuhimu wa kuundwa kwa chombo huru kitakachojumuisha wawakilishi kutoka taasisi za kimataifa zinazohusika na haki za binadamu na utawala bora, asasi za kiraia zilizo huru na majaji wenye rekodi ya kuaminika wanaoweza kusimamia haki bila kujichagulia upande,” imeeleza taarifa ya chama hicho, iliyosaniwa na Mohamed Ngulangwa, mkurugenzi wa habari.

Amesema, chama chake kinatahadharisha kuwa suala la kuwa na tume huru ya uchunguzi lisichukuliwe kwa uzito mwepesi na mzaha usipewe nafasi.

“Watu wengi wamepoteza maisha na watu wengi wamepoteza ndugu zao; uharibifu mkubwa wa mali za umma na binafsi umetokea na uchaguzi umevurugwa na kusababisha matokeo yaliyotangazwa kutoaminika,” amefafanua.

Anasema, “Tume inayopaswa kuchunguza matukio haya inapaswa kuwa huru na kuaminika ndani na nje ya nchi, kama kweli tuna lengo la kuliponya taifa.”

Nacho chama cha ACT-Wazalendo, kimepinga kuundwa kwa tume hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho, iliyotolewa na katibu mkuu wake, Ado Shaibu, ACT-Wazalendo, “kinapinga na kinakataa kabisa, tume iliyotangazwa na Rais Samia.”

Katibu mkuu wa ACT- Wazalendo anasema, “baadhi ya wajumbe wanaounda tume hiyo, wanapaswa kuwa sehemu ya uchunguzi huo badala ya wao kuchunguza.”
Ameongeza, “si chochote, nidhihaka kwa waliopoteza maisha yao, majeruhi na familia zilizofiwa katika matukio haya ya kinyama.”

About The Author

error: Content is protected !!