November 10, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Heche, Lema, Golugwa na Jacob, waachiliwa kwa dhamana

 

VIONGOZI wandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, wameachiwa kwa dhamana. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Mbali na Heche, wengine waliochiwa huru, ni Amani Gulogwa, Naibu Katibu Mkuu; Godbless Lema, Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Boniface Jacob, mwenyekiti wa Kanda ya Pwani.

Taarifa za kuachiwa kwa viongozi hao wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, zimethibitishwa na Gaston Garubindi, Mkurugenzi wa Sheria wa Chadema.

Heche alikamatwa tarehe 22 Oktoba 2025, kwenye geti la Mahakama Kuu, jijini Dar es Salaam, alipokwenda kusikiliza kesi ya uhaini, inayomkabili mwenyekiti wake, Tundu Lissu.

Tangu kukamatwa kwake, hadi anachiwa kwa dhamana, Heche alishikiliwa kwenye vituo vya Polisi vya Mburahati, jijini Dar es Salaam na Mtumba, mkoani Dodoma.

Alirejeshwa Dar es Salaam, tarahe 4 Novemba 2025. Mwanasheria wa Chadema, Hekima Mwasipu, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema, Heche anatuhumiwa kwa makosa ya ugaidi, yanayotokana na maandamano ya kupinga uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba mwaka huu.

Viongozi wengine wa Chadema waliokuwa wanashikiliwa na polisi, walikamatwa kuanzia tarehe 7 Novemba, muda mfupi baada ya jeshi hilo, kuwataka wajisalimishe.

Mbali na Jacob, Lema na Golugwa, wengine waliotakiwa kujisalimisha, ni pamoja na John Mnyika, Katibu Mkuu; Deogratius Mahinyila, Mwenyekiitiwa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) na Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano.

Katika orodha hiyo, wamo pia mbunge wa zamani wa Kawe na Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM); Askofu Josephat Gwajima, naibu mkuu wa makanisa hayo, Machumu Maximillian Kadutu (Askofu Mwanamapinduzi); Hilda Newton na Award Kalonga.

Golugwa alikamatwa nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, huku Lema akikamatwa maeneo ya Usa Rive, jijini Arusha. Jacob alikamatwa maeneo ya Goba, wilayani Ubungo.

About The Author

error: Content is protected !!