MAKAMU mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche, amekimbizwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam, baada ya hali yake ya kiafya kuripotiwa kudorora. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa zilizothibitishwa na mmoja wa wanafamilia wa mwanasiasa huyo zinasema,
Heche alichukuliwa kwenye kituo cha polisi cha Mburahati na kukimbizwa hospitali, kutokana na kukabiliwa na maradhi.
Haijaelezwa kipi hasa kinachombua, lakini kuna wakati MwanaHALISI liliwahi kuripoti kuwa Heche alikuwa akipatiwa matibabu nje ya nchi.
Mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, alikamatwa na polisi, mjini Dar es Salaam, wiki mbili zilizopita na kusafirishwa hadi mkoani Dodoma, kabla ya kurejeshwa Dar es Salaam, katikati ya wiki hii.
Jeshi la polisi liliwahi kueleza kuwa Heche anashikiliwa kutokana na maelekezo ya Idara ya Uhamiaji, waliokuwa wakimtuhumu kuondoka nchini Tanzani, bila kufuata taratibu za uhamiaji.

Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle, alinukuliwa akieleza kuwa Heche aliondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Kenya, katika Kituo cha Uhamiaji cha mpaka wa Sirari mkoani Mara, bila kufuata taratibu na kanuni za uhamiaji.
Hata hivyo, makamu mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini, amekana madai hayo na kusema, safari yake ya Kenya ilizuiwa ilizuiliwa na mamlaka za serikali ya Tanzania, katika Mpaka wa Isibania, na paspoti yake kuchukuliwa.”
Heche alitaka kwenda nchini Kenya, kuhudhuria mazishi ya kiongozi wa upinzani nchini humo, Raila Amollo Odinga, aliyemtaja kuwa alikuwa rafiki na mshirika mkubwa wa Chadema, pamoja na mshauri wake binafsi katika masuala mengi ya kisiasa.
Tangu kukamatwa kwake, takribani siku 15 zilizopita, Heche bado anazuiliwa na polisi. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu ijayo, akituhumiwa kuchochea maandamano ya uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba.
Katika hatua nyingine, mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, Godbless Lema, amekamatwa mjini Arusha.

Lema amekamatwa maeneo ya Usa River, akiwa na dereva wake na alichukuliwa na kupakiwa kwenye gari aina ya Alphad, iliyochukua muelekeo wa kuelekea mjini Moshi.
Kukamatwa kwa Lema, kumekuja baada ya jeshi la polisi kutangaza kuwatafuta watu 10 wengi wao wakiwa viongozi wa Chadema.
Mbali na Lema, wengine waliotajwa kwenye taarifa hiyo, ni John Mnyika, katibu mkuu wa chama hicho; Amani Golugwa, naibu katibu mkuu Bara; Boniface Jacob, mjumbe wa kamati kuu; Brenda Rupia, katibu wa uenezi na Deogratius Mahinyila, mwenyekiti wa baraza la vijana.
Wengine waliotajwa na polisi kuwa wanatafutwa, ni aliyekuwa mbunge wa Kawe na Mkuu wa Makanisa ya Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima.
Gwajima ni mmoja wa wakosoaji wakubwa wa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassana, hasa katika uminyaji wa demokrasia na kushamiri kwa vitendo vya utekaji, utesaji na mauaji nchini.
Aidha, jeshi la polisi limemtaja Askofu Maxmillian Machumu, naibu Katibu Mkuu wa Makanisa Ufufuo na Uzima na kiongozi wa Chadema mkoani Simiyu, kuwa miongoni mwa wanaowasaka.
Wengine wanaosakwa, ni Award Kalonga na mwanaharakati Hilda Newton.
Hata hivyo, viongozi wa Chadema, wanakana madai ya kuchochea vurugu. Wanasema, ajenda ya Chadema ya No Refoms, No Election – “Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi,” ni kauli ya kisiasa, inayolenga kushinikiwa kuwapo mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi nchini.
Katika maandamano yaliyodumu kwa siku tatu kuanzia 29 Oktoba 2025 – siku ya uchaguzi mkuu, watu kadhaa wamepoteza maisha huku mali za umma na binafsi zikaharibiwa.
Waandamanaji walikuwa wakitaka mabadiliko mbalimbali ikiwemo mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki lakini mamlaka nchini Tanzania sinadai maandamano hayo yalikuwa kinyume cha sheria na yaligubikwa na ghasia na uharibifu.
Bado taarifa rasmi haijatolewa kuhusu tathimini ya madhara yaliyotokea kutokana na maandamano hayo makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini, tangu kupatikana kwa uhuru wake, miongo ya sita iliyopita.
Taarifa mbalimbali za ndani na nje ya Tanzania ikiwemo wapinzani, wanaharakati na wanadiplomasia zinaeleza kuwa mamia ya watu wameuawa na vyombo vya usalama ikiwemo polisi. Serikali imekanusha madai hayo.
Maandamano hayo yaliyoanzia jijini Dar es Salaam, yalisambaa kwa kasi katika maeneo mengine ikiwemo majiji ya Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma.
Katika baadhi ya maeneo, maandamano hayo yaliyoratibiwa na mwanaharakati wa mitandaoni, Mange Kimambi, yamesababisha uharibifu mkubwa, ikiwamo kuchomwa moto kwa vituo vya polisi, ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), vituo vya mafuta, migahawa na maduka kadhaa.
ZINAZOFANANA
Watu 172 kortini kwa kufanya vurugu, unyang’anyi siku ya Uchaguzi
Gwajima vigogo Chadema wasakwa na Polisi
Niffer, GEN Z washtakiwa kwa uhaini