November 7, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Niffer, GEN Z washtakiwa kwa uhaini

Jeniffer Jovin 'Niffer'

 

WATU 98 akiwemo Jeniffer Jovin ‘Niffer’, mfanyabiashara maarufu wa vipodozi nchini, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini, yanayohusishwa na maandamano ya uchaguzi wa 29 Oktoba 2025. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Niffer na wenzake wamefunguliwa kesi namba 26388/2025 leo tarehe 7 Novemba 2025 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, watuhumiwa 76 kati yao wanashitakiwa kwa makosa mawili ya kula njama ya kutekeleza uhalifu, kinyume na kifungu cha 384, cha sheria ya kanuni ya adhabu ya 2023.

Katika shtaka la pili, washitakiwa wanatuhumiwa kwa uhaini kinyume na kifungu cha 39 (2) (d) cha sheria ya kanuni ya adhabu ya 2023.

Aidha, watuhumiwa wengine 21 wanashitakiwa kwa mashitaka mawili – kula njama ya kuharibu miundo mbinu na uhaini.

Wamesomewa mashitaka hayo leo, Ijumaa tarehe 7 Novemba 2025, wakidaiwa kutenda makosa hayo, kati ya tarehe 1 na 29 Oktoba.

Wamesomewa mashtaka yao na wakili wa serikali mwandamizi Clemence Kato, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, watuhumiwa wakiwa na chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wakiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikusudia kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kwa lengo la kutishia serikali na walidhihirisha dhamira hiyo kwa kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za serikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.

Watu hao wanatuhumiwa kutenda makosa hayo katika maeneo mbalimbali ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Jenipher pamoja na mashtaka hayo, anatuhumiwa kwa uchochezi wa kuhamasisha umma kununua barakoa za kuzuia moshi wa kutoa machozi, wakati wa maandamano ya kupinga uchaguzi wa 29 Oktoba 2025.

Anatuhumiwa kutenda kosa hilo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kati ya tarehe 1 Agosti na 24 Oktoba mwaka huu.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania mashtaka ya uhaini hayana dhamana na adhabu yake kwa atakayekutwa na hatia ya kosa hilo ni kifo.

Katika maandamano yaliyodumu kwa siku tatu kuanzia 29 Oktoba 2025, siku ya uchaguzi, watu kadhaa wamepoteza maisha, wakitaka mabadiliko mbalimbali ikiwemo mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki.

Watuhumiwa hao ni pamoja na Paulina Palango, Justine Suguta Lawrance, Moses Ngao, Simon Makaranga Joshua, Job Thomas, Bernadetha Laizer, Benidicto Kwendesha na John Mwakimi.

Wengine, ni Suzan Mkami, Jackson Mwirenga, Julitha Shirima, Julieth Tilya, Hussein Salehe, Robert Urio ‘Njaakali’, Ridhiki Amiri, Godwin Bweni, Alphas Joseph, Thabit Katusi na Timothy Mlengela.

Katika orodha hiyo, wamo pia Aron Daud, Pual Miren, Shaban Salim, Christopher Chacha Nsemba, Kelvin Sawe, Masumbuko Tungu, Simon Kota, Peter Pesambili , Hamis Halifa, Salvatory Mushi, Liston Chacha, Said Ngoma, Emmanuel Meteli, Joseph Msumari na Sharifa Mohamed Seleman.

Wengine, ni Kisesa Ulimwengu, Witness Mboya, Sigule Maletelwa, Maiko Stoko, Yokitan Bwayonga, Said Salehe Abdallah, Japhet Samweli, Hussein Abdu Saidi, Japhari Sala, Edison Andrea, Ronaldo Tarimo, Paskali Jonathan, Oscar Khumbe

Wamo pia, Joseph Thomaso, Enock Chacha, Huseni Mahamud Bakari, Abdul Fadhili Ally, Japheti Samweli, Khalid Juma, Joseph Peter, Thomas Mollel na Brayson Masunga.

About The Author

error: Content is protected !!