RAIS wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), wakili Boniface Mwabukusi, amelaani vikali hatua ya Jeshi la Polisi na kumkamata na kumfungulia jalada la tuhuma za ugaidi Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).
Mwabukusi amesema hatua hiyo ni kinyume cha sheria na inalenga kukandamiza demokrasia nchini.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Mwabukusi ametoa taarifa hiyo akieleza hatua hiyo ni ‘kumwaga petroli kwa kudhania unazima moto’ kwa kumhusisha Heche na tuhuma za ugaidi.
“Ni upuuzi kumtuhumu John Heche kwa ugaidi. Hali ya usalama siyo nzuri kuendelea na desturi za kupika kesi ili kubambika watu, mnatia aibu taaluma na mnakera,” ameandika Mwabukusi.
Mwabukusi amedai kuwa Heche alikamatwa na kuzuiliwa kinyume cha sheria na kwamba ni wakati wa Mahakama kukataa kutumika kama “kokoro la kutekeleza uhalifu dhidi ya demokrasia” na kutaka polisi na Ofisi ya DPP wadhibitiwe akisema kuwa vyombo hivyo vinataka “kulipua moto ambao hautazimika”.
Kiongozi huyo wa TLS amesema chama hicho kitatoa msaada wa kisheria kwa Heche, pamoja na familia zilizodhulumiwa au kujeruhiwa wakati wa maandamano yaliyosababisha vifo na majeraha kwa vijana.
“Tuliwaonya kwa sauti, tukawafuata kwa unyenyekevu mkubwa na kuwaambia hawa vijana wa sasa siyo wale ambao hatuku-reason na niliwaambia kwamba halahala kidole na jicho…acheni vijana hawa, wametulia kidogo kwasababu wana busara kuliko sisi, tusiwachokoze”, ameandika Mwabukusi.
ZINAZOFANANA
Watahiniwa 937,581 wafaulu elimu ya msingi
Rais Samia amuapisha Mwanasheria Mkuu
Musiba akimbia siasa za upinzani, CCM