MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa Tanzania Bara zitakazotumika kuanzia leo tarehe 5 Novemba 2025 ambapo katika Bandari ya Dar es Salaam petroli itauzwa kwa Sh. 2,752 kwa lita, Tanga Sh. 2,813 na bandari ya Mtwara kwa Sh. 2,844 kwa bei ya rejareja kwa lita. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Dizeli itauzwa kwa Sh. 2,704 katika Bandari ya Dar es Salaam, Sh. 2,766 Bandari ya Tanga na Sh. 2,797 katika Bandari ya Mtwara.
Katika Mkoa wa Dodoma, Petroli itauzwa Sh. 2,831 kwa lita, dizeli Sh. 2,783 kwa lita, wakati Arusha Petroli itauzwa Sh. 2,861 na Dizeli Sh. 2,814 kwa lita na Mwanza Petroli itauzwa Sh. 2,937 na Dizeli itauzwa Sh. 2,890 kwa lita na Mbeya Petroli itauzwa kwa Sh. 2,884 na Dizeli itauzwa kwa Sh. 2,837 kwa lita.
EWURA imewataka wafanyabiashara wote wa bidhaa za mafuta ya petroli kwa rejareja na jumla kuuza mafuta kwa bei zilizotangazwa na mamlaka hiyo na atakayekiuka agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuchuliwa dhidi yake.
Pia, imevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta ya petroli katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika ili pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja waweze kununua bidhaa hizo katika vituo vinavyouza kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.
Kwa mujibu wa EWURA, kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja ni kosa na adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.
Aidha, EWURA imewataka wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye ‘Electronic Fiscal Pump Printers’ (EFPP) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
ZINAZOFANANA
Watahiniwa 937,581 wafaulu elimu ya msingi
Mwabukusi alaani Heche kutuhumiwa kwa ugaidi
Rais Samia amuapisha Mwanasheria Mkuu