October 3, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Uchaguzi wa Ubunge Fuoni kufanyika Desemba 30

 

UCHAGUZI wa Ubunge katika Jimbo la Fuoni, Zanzibar na Udiwani katika Kata ya Chamwino mkoani Morogoro na Kata ya Mbagala Kuu mkoani Dar es Salaam utafanyika siku ya Jumanne tarehe 30 Desemba 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kufanyika kwa uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Fuoni kwa tarehe hiyo kufuatia kifo cha Abass Ali Mwinyi, aliyekuwa mgombea wa Ubunge Jimbo la Fuoni Wilaya ya Magharibi B, Zanzibar, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichotokea tarehe 25 Septemba 2025.

Kwa udiwani ni kufuatia kifo cha Hassani Salum Hassani, aliyekuwa mgombea wa Udiwani katika Kata ya Chamwino, Jimbo la Morogoro Mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kilichotokea tarehe 27 Septemba 2025 na kifo cha Rajabu Sultan Mwanga, aliyekuwa mgombea Udiwani Kata ya Mbagala Kuu, Jimbo la Mbagala, Dar es Salaam kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kilichotokea tarehe 27 Septemba 2025.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima imeeleza kuwa fomu za uteuzi kwa mgombea Ubunge Jimbo la Fuoni kupitia CCM na wagombea Udiwani katika Kata ya Chamwino na Kata ya Mbagala Kuu kupitia CUF zitatolewa kuanzia tarehe 15 Oktoba 2025 hadi tarehe 21 Oktoba 2025, na uteuzi wa mgombea Ubunge Jimbo la Fuoni na wagombea Udiwani katika Kata ya Chamwino na Kata ya Mbagala Kuu utafanyika tarehe 21 Oktoba 2025.

Kampeni za uchaguzi wa Ubunge Jimbo la Fuoni zitafanyika kuanzia tarehe 22 Oktoba 2025 hadi tarehe 27 Oktoba 2025, na tarehe 28 Oktoba 2025 hadi tarehe 4 Novemba 2025 zitasitishwa ili kupisha upigaji kura ya mapema kwa upande wa Zanzibar na siku ya kupiga kura hadi kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu tarehe 29 Oktoba 2025.

Muda wa kampeni za uchaguzi huo umepangwa kufanyika kuanzia tarehe 5 Novemba 2025 na kumalizika tarehe 29 Desemba 2025.

About The Author

error: Content is protected !!