September 24, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Samia aweka shada la maua kaburini kwa Mkapa

 

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, leo Jumatano tarehe 24 Septemba 2025, ameweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, huko Lupaso, wilayani Masasi mkoani Mtwara. Anaripoti Zakia Nanga, Masasi … (endelea).

Samia yuko mkoani Mtwara anakoendelea na shughuli zake za kampeni za kusaka kurejea tena Ikulu, katika uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba mwaka huu.

Benjamin William Mkapa, aliongoza serikali kati ya Novemba 1995 hadi Desemba 2005, akiwa rais wa kwanza aliyechaguliwa katika uchaguzi ulioshirikisha vyama vingi vya siasa nchini.

Mfumo wa vyama vingi ulirejea nchini mwaka 1992. Mkapa alizaliwa wilayani Masasi, mkoani Mtwara, tarehe 12 Novemba 1938 na kufariki dunia, tarehe 24 Julai 2020.

Katika Kongamano la Maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa kiongozi huyo, tarehe 14 Julai 2021, Rais Samia alinukuliwa akisema kwamba kitabu cha historia ya Tanzania hakiwezi kukamilika bila kuwepo kwa sura nzima yenye kumwelezea Hayati Mkapa na mageuzi mengi aliyoyafanya katika uongozi wake.

Aidha, Rais Samia alisema kwamba Hayati Mkapa ndie aliyeanzisha taasisi nyingi nchini ambazo bado zinaendelea kufanya kazi nzuri mpaka leo.

Alizitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF).

Nyingine ni Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKURABITA) na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS).

Kwa upande wa maendeleo ya uchumi wa nchi kwa ujumla, Rais Samia alisema, Hayati Mzee Mkapa alifanikiwa kupunguza deni la Taifa kutoka asilimia 143.7 mwaka 1995 hadi asilimia 60.7 mwaka 2005.

Anasema, mafanikio ya Mkapa yalichochewa na uwezo wake wa kidiplomasia katika kuzishawishi taasisi za kifedha za kimataifa na nchi wahisani kusamehe madeni yao kwa kutumia mpango wa Heavily Indebted Poor Countries (HIPC) ,uliosimamiwa na Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF).

About The Author

error: Content is protected !!