
MAJERUHI wawili kati ya 11 waliokuwa wakipatiwa matibabu kufuatia ajali ya basi la abiria na lori iliyotokea Chemba, mkoani Dodoma, wamefariki dunia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Kufariki duni kwa majeruhi hao, kumefikisha idadi ya vifo kwenye ajali hiyo, kufikia watu kumi na moja.
Ajali hiyo ilitokea alfajili ya jana Alhamisi, tarehe 18 Septemba 2025, na kusababisha vifo vya watu tisa, watano wanaume na wanne wanawake.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma, Dk. Ernest Ibenzi, amesema kwamba majeruhi hao wawili wamepoteza maisha, wakati wakipatiwa matibabu.
“Jana tulipokea majeruhi tisa, baadaye waliletwa wengine wawili waliokuwa wamefanyiwa upasuaji katika hospitali ya Wilaya ya Chemba. Kwa bahati mbaya hawa ndio walipoteza maisha,” amefafanua.
Miongoni mwa waliofikishwa hospitalini, Ibenzi amesema, ni mtoto mdogo wa umri wa chini ya mwaka mmoja ambaye ndugu wameshamtambua na kumtaja mama yake kuwa ni miongoni mwa majeruhi tisa waliofikishwa hospitalini akiwa hajitambui.
Aidha, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma wa hospitali hiyo, Renatha Mzanje amesema, miongoni mwa waliofariki ni mwanamke anayekadiriwa kuwa na miaka thelathini na tano.
Kuhusu mtoto, Mzanje amesema, “Wakati anapata ajali alikuwa na mama yake mzazi ambaye amelazwa hapa, lakini bado hali yake siyo nzuri. Ndugu wameshafika na wamemtambua. Kwa sasa anaendelea na matibabu.”
Ajali ya basi la abiria na lori ilitokea jana alfajiri, tarehe 18 Septemba, katika eneo la Kambi ya Nyasa, wilayani Chemba mkoani Dodoma. Watu watano walifariki hapo hapo na wengine wanne, walifariki dunia wakiwa wanapelekwa hospitali. Watu wengine 16 wamejeruhiwa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, alisema kuwa chanzo chake ni uzembe wa dereva wa lori aliyehama upande wake wa kushoto na kwenda kulia, kulikosababisha magari hayo kugongana uso kwa uso.
Basi lililopata ajali linamilikiwa na kampuni ya Abuu Trans na kwamba basi lilikuwa likitoka wilayani Kondoa kwenda Dodoma, huku lori likitokea Dodoma kwenda Kondoa.
Miongoni mwa waliopoteza maisha ni wanafunzi wanne aliowataja kuwa ni Carolyne Joachim (13), Rukia Ally (14), Bashir Hashim (13) na Nasra Mohamed (18).
Dereva wa lori ni miongoni mwa majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu.
ZINAZOFANANA
Meridianbet yaendeleza harakati za usafi hospitali ya Mwenge
Masista waliofariki ajalini yaagwa leo, watatu wazikwa mmoja kusafirishwa
Polepole awapa somo jipya polisi