September 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

SBL, NCT wawawezesha vijana kupitia mafunzo ya ukarimu Arusha

 

KAMPUNI ya Bia ya Serengeti kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) wamezindua rasmi awamu ya pili ya programu ya Learning for Life katika Tawi la NCT Arusha. Wakitanua ushirikiano ulioanzishwa jijini Dar es Salaam tangu Septemba 2024. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Katika udahili huu wa Arusha, zaidi ya vijana 150 wataandikishwa na kupata mafunzo ya vitendo yanayolenga moja kwa moja ajira katika hoteli za kifahari na kawaida, migahawa na baa za kanda ya utalii ya kaskazini.

Awamu hii inakuja baada ya mafanikio ya kundi la kwanza lililoandikishwa Dar es Salaam ambapo wanafunzi 100 walihitimu mwezi Mei 2025. Utekelezaji huu wa Arusha umebuniwa ili kuwa wa kudumu na wenye tija, ambapo SBL imewekeza katika mfumo wa kuwafundisha wakufunzi (ToT) kwa wakufunzi wa NCT, hatua itakayokiwezesha chuo hicho kuendesha makundi yajayo kwa uhuru na uimara.

Hii inahakikisha upatikanaji wa uhakika wa vijana wenye ujuzi wa kazi kwa sekta ya ukarimu na utalii, sekta muhimu katika kukuza uchumi wa taifa.

Programu hii inachanganya darasa la nadharia na mafunzo ya vitendo kupitia eneo la kazi. Wanafunzi pia watanufaika na maudhui kutoka Diageo Bar Academy kuhusu uendeshaji wa baa, uandaaji wa vinywaji na huduma kwa wateja, sambamba na stadi muhimu za maisha kama vile mawasiliano, kujenga taswira ya kitaaluma na uongozi.

Matokeo yake ni kundi la vijana waliokamilika kitaaluma na kijamii, tayari kuinua viwango vya huduma na kuboresha uzoefu kwa wageni kuanzia siku ya kwanza ya ajira zao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey, aliongelea athari chanya za programu hiyo akisema:

“Programu hii imefungua milango mipya kwa wanafunzi wetu. Inawapa zaidi ya nadharia darasani kwa kuwapeleka kwenye mazingira halisi ya kazi, jambo linaloongeza kujiamini na kuwapa uwezo wa kukidhi matarajio ya waajiri katika sekta ya ukarimu na utalii. Tunajivunia kuendeleza ushirikiano huu na SBL hapa Arusha.”

Aidha, NCT inatangaza kwamba mafunzo ya muda mfupi chini ya programu ya Learning for Life yanatarajiwa kuanza tarehe 22 Septemba 2025 na kuhitimishwa tarehe 02 Novemba 2025. Gharama zote za mafunzo haya zitagharamiwa na Serengeti Breweries Limited (SBL), huku wanafunzi wakigharamikia malazi, chakula na usafiri.

Waombaji wanatakiwa kutuma fomu za maombi kabla ya tarehe 16 Agosti 2025. Fomu za maombi zinapatikana kupitia tovuti ya Chuo: www.nct.ac.tz au katika ofisi za kampasi za NCT zilizopo Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.
Sifa za mwombaji:
•⁠ ⁠Awe Mtanzania.
•⁠ ⁠Awe na barua ya utambulisho kutoka Serikali ya Mtaa/Kijiji au kutoka kwa mwajiri.
•⁠ ⁠Awe na umri kati ya miaka 15 – 35.
•⁠ ⁠Awe mwenye afya njema.
•⁠ ⁠Awe na elimu ya Cheti au zaidi katika fani ya Ukarimu na Utalii.

Naye Mkurugenzi wa Mauzo wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Bw. Christopher Gitau, aliongeza; “Sisi kama SBL tunaamini kwamba kuwekeza kwa vijana ni kuwekeza kwenye mustakabali wa jamii zetu. Kupitia Learning for Life tunawapa stadi za kiufundi lakini pia tunawajengea uwezo wa kuwa viongozi, wajasiriamali na wachangiaji wakuu wa ukuaji wa sekta ya ukarimu na utalii nchini.”

Programu ya Learning for Life ni sehemu ya ajenda ya kijamii ya SBL, Spirit of Progress, ikidhihirisha dhamira yake ya muda mrefu ya kuwekeza kwa jamii, kujenga uwezo na kuwawezesha vijana wa Kitanzania. Kupitia upanuzi huu Arusha, programu hii itatoa njia mpya za ajira na kuimarisha zaidi sekta ya utalii na ukarimu nchini Tanzania.

About The Author

error: Content is protected !!