September 1, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mwendokasi Mbagala bado kuzungumkuti

USAFIRI wa mabasi yaendayo haraka, maarufu kama Mwendokasi, uliotarajiwa kuanza leo, tarehe 1 Septemba 2025, katika barabara ya Mbagala, umesogezwa mbele, kufuatia kutokamilika kwa baadhi ya miundombinu. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dk. Athuman Kihamia amesema, kuchelewa kuanza kwa huduma hiyo, kumesababisha na kutokamilika kwa baadhi ya miundombinu ikiwamo mageti, katika kituo cha kujazia gesi.

Amesema, tayari mabasi hayo yameshawasili nchini, lakini yameshindwa kuanza kazi kutokana na mapungufu hayo.

Hata hivyo, Kihamia amesema, taarifa rasmi kuhusu maendeleo ya ujenzi huo wataitoa baada ya wiki moja.

“Mabasi yamewasili, lakini hatutaweza kuanza kutoa huduma leo kama tulivyoahidi kwa kuwa baadhi ya miundombinu haijakamilika,” alifafanua Kihamia.

Akaongeza, “mageti janja kwa ajili ya ukataji wa tiketi bado hayajafungwa na kituo cha kujazia gesi kilichopo kwenye karakana ya Mbagala nacho hakijakamilika.”

Mabasi hayo 151 yaliwasili katika karakana ya Mbagala Rangi Tatu usiku wa tarehe 29 Agosti, baada ya kutoka bandarini, shughuli iliyochukua takribani siku mbili.

Awamu ya kwanza ya mabasi yaendayo haraka yatakayotoa huduma katika awamu ya pili ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) yamewasili nchini, huku baadhi ya miundombinu ikiwa haijakamilika na mingine ikianza kuharibika.

Mabasi hayo yaliyolewa nchini na kampuni ya Mofat, ni sehemu ya yale 250 yatakayotoa huduma katika njia hiyo, yametengenezwa nchini China.

Njia yatakayotoa huduma, inahusisha barabara ya Mbagala hadi Gerezani yenye urefu wa kilomita 20.3, iliyojengwa na kampuni ya Sinohydro ya China, na ilikabidhiwa kwa DART tangu Agosti 2023.

Katika awamu hiyo, kampuni ya Mofat ndiyo imepewa mkataba wa miaka 12 kutoa huduma hiyo, na mabasi yake yatatumia nishati ya gesi asilia.

About The Author

error: Content is protected !!