September 1, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Majemedari Zbar wakabana

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman

 

WAKUU wa vyama vinavyoshindania udhibiti wa siasa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi na Othman Masoud Othman sasa wanakabana katika kutafuta ridhaa ya wananchi ya kuiongoza Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Baada ya Dk. Mwinyi anayemaliza miaka mitano ya uongozi wa serikali, kuchukua fomu ya uteuzi Jumamosi, Othman alifika jana makao makuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar [ZEC], Maisara mjini hapa na kama ilivyo, kukabidhiwa fomu hiyo na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji George Joseph Kazi.

Dk. Mwinyi aliingia Ikulu ya Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa 2020 uliolalamikiwa kuwa ulichafuliwa kwa faida ya Chama Cha Mapinduzi [CCM], baada ya kutangazwa mshindi ndani ya malalamiko kuwa Maalim Seif Shariff Hamad aliyewakilisha Chama cha ACT Wazalendo, ameendelea kudhulumiwa.

Safari hii nguvu ya ushindani japo inaonekana kama iliyopoza kwa sababu ya upya kisiasa wa Othman Masoud, ni matarajio ya walio wengi kuwa hwenda ikawa ndio kheri kwa umma uliohitaji mabadiliko ya uongozi kwa miaka mingi chini ya mfumo wa vyama vingi.

Dk. Mwinyi alisindikizwa na msafara mkubwa uliopambwa na maaskari wa polisi, usalama na vikosi vya SMZ wakizunguka makundi ya viongozi waandamizi wa CCM, wafuasi na wapita njia waliojipanga pembeni mwa barabara kutokea Kilimani, Miembeni hadi kufika Ofisi Kuu za CCM Kisiwandui.

Lakini tamasha hasa la hafla ya uchukuaji wa fomu lilikuwa uwanja wa Mao Tse Tungu, Kikwajuni.

Othman yeye akifuatana na msafara ulioongozwa na Kiongozi wa Chama [KC], Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti Zanzibar Ismail Jussa Ladhu, Wajumbe wa Kamati Kuu na wakuu wa chama kutoka mikoa yote mitano ya Zanzibar, akipambwa na rangi ya zambarau, alikabidhiwa fomu akiwa mgombea mpya baada ya kujiunga kwenye siasa mwaka 2021 akimrithi Maalim Seif, jemedari aliyeasisi harakati za kuiangusha CCM. Maalim Seif alifariki dunia tarehe 19 Februari 2021.

Dk. Hussein Ali Mwinyi

Kwenye hotuba zao mbele ya halaiki iliyokusanyika kuwashuhudia washindani wakubwa hawa, Dk. Mwinyi alipalilia kuendelea kuaminiwa kwa urais akiringia mafanikio ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo aloifanikisha.

Hakutaka kusema sana akieleza kuwa wakati wa kampeni bado, lakini dhahiri hakustahamili kuonesha hasira dhidi ya kile alichoeleza “wale wenzetu hawaelezi watawafanyia nini wananchi isipokuwa wao ni kutukana tu.”

Anasema: Leo mkusanyiko wetu huu mkubwa si wa kampeni. Muda ukifika tutaelezana mambo yetu kwa kuonesha mafanikio. Na tutafanya kampeni za kistaarabu haijapata kutokea. Sio kama wenzetu ambao huoni wanaeleza sera isipokuwa kutukana tu.”

Kwa Othman, mtaalam mbobezi wa sheria na katiba na mkamo wa kwanza wa rais tangu Februari 2021, akizungumza na umma uliokusanyika mbele ya Ofisi Kuu ya chama Vuga, alisema sasa wamedhamiria hasa kujipanga kwa ajili ya kuiongoza Zanzibar.

“Muda umefika sasa, na kwa dhati ya moyo wangu ninawashukuru sana kwa kuniamini mkanikabidhi dhamana hii kubwa kutoka kwa tuliyemzoea na tukimpenda sana. Tujiandae kwa uchaguzi wa haki Januari mwakani. Nitahakikisha tunaunda serikali na kuondokana na uongozi huu usiojali maslahi yenu na Zanzibar yenu,” alisema.

Othman anayejinasibu kufundishwa uongozi na uzalendo wa nchi na viongozi wenye maono, anasema ni fedheha leo Zanzibar kushikwa na watu aliodai wana agenda za siri wakiitafuna nchi kwa visingizio vya miradi ya maendeleo.

Anasema, “Hawa weshashindwa uchaguzi. Wanasema kura ya siku mbili wanayojua haiwasaidii kuzishinda imani zenu Wazanzibari mkawachagua. Nchi ni kama imetekwa nyara, Kiongozi unachukua ndugu zako wanashika vikosi (huku Wazalendo) wenyewe wanaangalia. Hawataki na wanajua wanachokitaka kuhusu nchi yao yenye historia ya kuwa na kikosi cha Polisi tangu mwaka 1908.”

Akiendelea kuonesha upinzani mkali dhidi ya uchaguzi wa siku mbili, Othman kwanza aliutaja kuwa unaotokana na “Sheria ya kijinga” halafu akasema unazidi kupingwa kwa sababu anaona si uchaguzi chochote bali “uchochoro wa kuiba kura.”

“Kura ya mapema ni wizi wa mapema, ni upenyo wa kuhalifu maamuzi yenu. Sasa sisi tutatangulia hii siku ya kwanza tuwasaidie. Sikieni sote tutatoka siku hiyo. Ndio njia ya kupinga sheria ya kijinga,” alisema akimtaja Trevor Noah, chotara wa Afrika Kusini kutokana na mama wa Kiswizi aliyeolewa na baba yake Muafrika mweusi.

Kupitia kitabu chake cha “Born A Crime” ikimaanisha mzaliwa katika uhalifu wa sheria ovu, Othman aliasa wana ACT wakaze kamba kupigania ushindi wakijua kwa uhakika kuwa wanategemewa sana na wengi upande wa CCM “waliochoka kuongozwa kwa jeuri na kunyanyaswa kwenye nchi yao.”

Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar, muda wa kukamilisha masharti ya kuomba uteuzi kwa wagombea urais, utakwisha tarehe 10 Septemba ambako fomu ziwe zimerudishwa ifikapo Saa 10 laasir. Uteuzi utatangazwa siku inayofuata hapohapo zikifuata siku 45 za kampeni kufikia tarehe 28 kura ya mapema.

About The Author

error: Content is protected !!