
Jakaya Kikweye
RAIS mstaafu Jakaya Kikwete amesema, watu wanaopinga mchakato wa kumteua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais wanajifanya hamna nazo na wana roho ya korosho. Anaripoti Salehe Mohamed, Dar es Salaam … (endelea).
Amesema, watu wanajifanya hamnazo kwa kupinga jambo ambalo kila miaka limekuwa likifanyika ndani ya chama hicho bila matatizo.
Kikwete ametoa kauli hiyo leo, tarehe 28 Agosti 2025, wakati akihutubia maelfu ya wananchi, katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, jijini Dar es Salaam. Ni katika ufunguzi wa kampeni za uchuguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 29 Oktoba.
Amesema, baadhi ya wanaopinga uamuzi wa mkutano mkuu wa 19 Januari mwaka huu, wamo ndani ya chama hicho kwa miaka mingi na wanajua utaratibu wa uteuzi.
“Utaratibu na utamaduni wa CCM, kama Rais aliye madarakani amehudumu kwa kipindi kimoja basi huachwa amalizike kipindi cha pili cha uongozi,” alieleza.
Aliongeza, “Mimi ninalumiwa kwa namna nilivyosema kwenye mkutano mkuu wa kumchagua Rais Samia, Dk. Mwinyi (Hussein Ali Mwinyi, mgombea urais wa Zanzibar) na Dk. Emmanuel Nchimbi, kuwa mgombea mwenza. Wanaopinga uteuzi huo, wanajifanya kama hawafahamu utaratibu wa kwetu, labda kama wamesahau tuwakumbushe, lakini wengine wanafahamu lakini wanajifanya hamnazo.”
Kikwete alidai kuwa “CCM kuna utaratibu Rais aliyepo madarakani anapotaka awamu ya pili anapewa fursa bila kushindanishwa na yoyote. Tulifanya hivyo kwa Benjamani Mkapa, ilikuwa hiyo kwangu, ikawa hivyo kwa Rais John Magufuli. Kwa nini kuna kelele na iwe tofauti kwa Rais Samia,” amehoji
Amesema, “Sababu ya haya yote ni nini? Mbona haya hatukuyasikia kwa Kikwete, Mkapa, Kikwete? Wenye kimbelembele wao wenyewe walikuwapo wakati wa marais wote, kwa nini iwe sasa.Wanataka kuwatia wana CCM na Watakanzania yakayamoyo kwa jambo ambalo halipo.”
Kauli hiyo ya Kikwete ni kama vile anamjibu kada wa chama hicho Dk. Godfrey Malisa, aliyefungua kesi ambayo hata hivyo imetupwa na aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, anayedai kuwa kilichofanyika ni kunajisi katiba, taratibu na miongozi ya chama.
Polepole alitaka CCM kujisahihisha kwa kurudia mchakato huo kwa kuwa kikao kilichompitisha hakikuwa na jukumu hilo.
Aidha, Polepole anasema, Rais Samia hakustahili kugombea nafasi hiyo, kwa kuwa aliingia madarakani na Magufuli na kwamba muda wao wa uongozi unakoma Novemba mwaka huu.
Akifafanua hoja yake, Polepole anasema, “Mchakato wetu wa kumpata mgombea urais, umeharibu misingi ya uongozi, maadili, haki, utu na utamaduni.” Anataka mchakato urudiwe upya ili “chama kijisafishe na kuleta mgombea mwingine mwenye vigezo,” akisisitiza kuwa mgombea asiwe Samia Suluhu Hassan.
Polepole aliyejiuzuru wadhifa wa ubalozi, Julai mwaka huu, kwa madai kuwa hawezi kuwa sehemu ya serikali isiyojali misingi ya haki, sheria na katiba, anasema, Rais Samia alikuwa mgombea mwenza wa Magufuli. Waliingia madarakani miaka 10 iliyopita. “Anapaswa kuondoka Ikulu Oktoba mwaka huu, baada ya muhula wao wa uongozi kumalizika.”
Anaongeza, “…huu ni mwaka wa CCM kupeleka kwa wananchi, wagombea wapya. Rais, makamu wa rais na waziri mkuu wa sasa, hawapaswi kuwa warithi wa kiti cha urais, kwa vile ni sehemu ya uongozi unaomaliza muda wake.”
ZINAZOFANANA
Rais Samia kuunda tume ya maridhiano, upatanishi
Mahakama yakubali Chadema kumshitaki Msajili, yazuia kutowatambua viongozi wake
Pigo jingine ACT- Wazalendo lanukia