August 5, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

TRA, NCAA, TANAPA na TAWA kuunda kamati ya pamoja kuongeza mapato

 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) wameafikiana kuunda kamati tendaji ya pamoja itakayolenga kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Makubaliano hayo yamefikiwa leo, Agosti 4, 2025, katika kikao kilichoongozwa na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda kilichofanyika katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna Mwenda amesema lengo la kikao hicho ni kujadili namna bora ya kuongeza ushirikiano baina ya taasisi hizo, hasa katika kubadilishana taarifa zitakazosaidia kuboresha utendaji kazi na kuongeza makusanyo ya mapato ya serikali.

“Lengo la kikao hiki ni kubadilishana uzoefu na kujadili njia za kuboresha ukusanyaji wa kodi kupitia taasisi zetu…zote ni taasisi za serikali, na dhamira yetu ni kuitumikia serikali kwa ufanisi zaidi,” amesema Mwenda.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, akizungumza katika kikao cha viongozi wa TRA, TANAPA, NCAA na TAWA

Kamishna Mwenda ameongeza kuwa wamekubaliana kuunda kamati tendaji ya pamoja itakayorahisisha mawasiliano kati ya taasisi hizo ili kurahisisha utoaji wa taarifa muhimu, na kutatua changamoto mbalimbali kwa pamoja.

Kwa upande wake, Kamishna wa NCAA, Abdul-razak Badru, amesema kikao hicho ni mwanzo mzuri wa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi hizo, na kuundwa kwa kamati hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza tija katika utendaji kazi na mapato ya serikali.

“Ni mara ya kwanza kwa taasisi zetu kukutana kwa namna hii. Kuundwa kwa kamati hii kutaimarisha mabadilishano ya taarifa na hatimaye kusaidia kuongeza mapato ya serikali,” amesema Badru.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Kamishna wa TANAPA, Musa Kuji na Naibu Kamishna wa TAWA, Thabit Mkwaya, pamoja na viongozi waandamizi kutoka taasisi husika.

About The Author

error: Content is protected !!