July 27, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Biteko awaongoza washiriki 12,000 Mbio za NBC Dodoma Marathon, Mil 700 zakusanywa

 

NAIBU Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko leo ameongoza washiriki zaidi ya 12,000 wa mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma huku akiwapongeza waandaaji wa mbio hizo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kufanikiwa kukusanya fedha kiasi cha Sh. 700 milioni zitakazoelekezwa katika kufadhili malengo makuu matatu yenye dhima ya jumla ya kuokoa maisha ya mama na mtoto. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Katika mbio hizo zilizohusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, ilishuhudiwa washiriki kutoka Tanzania, Kenya na Uganda wakichuana vikali kwa kuibuka washindi kwenye mbio tofauti hususani zile za km 10, km 21 na km 42. Dk. Biteko aliwaongoza viongozi mbalimbali wakiwemo wa kitaifa na viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali walioshiriki kwenye mbio za KM 5.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi na wadau mbalimbali wa mbio hizo, Dk. Biteko pamoja na kuipongeza benki ya NBC kwa mafanikio hayo, alionyesha kuguswa na ongezeko kubwa la washiriki wa mbio hizo kutoka washiriki 1,500 mwaka 2020 hadi kufikia washiriki 12,000 waliojiandikisha rasmi kushiriki mbio hizo mwaka huu.Hatua hiyo alisema inasadifu mwamko mkubwa wa wananchi kushiriki katika michezo hatua ambayo itasaidia katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa moyo, kisukari na figo.

“Takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 33 ya Watanzania wanakabiliwa na changamoto ya uzito ulipitiliza huku asilimia 28 ya Watanzania wakikabiliwa na changamoto ya shinikizo la damu. Kwa takwimu hizo ukweli unabaki kuwa suala la mazoezi sio suala ya hiyari bali ni hitaji la lazima kwa mwili wa binadamu. Hii ndio sababu nawapongeza sana NBC na wadau wengine kwa jitihada zao za kubuni matukio ya michezo kama haya hongereni sana,’’ alipongeza

Dk. Biteko alioumba uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuzitambua rasmi mbio za NBC Dodoma Marathon kama kivutio rasmi cha utalii na kichocheo cha Uchumi katika mkoa huo kutokana na mchango wake katika kutangaza utalii wa mkoa huo sambamba na uchocheaji wake Uchumi wa wananchi kupitia mzunguko wa fedha utokanao na idadi kubwa ya wageni wanaotembelea jiji hilo ili kushiriki mbio hizo.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Paramagamba Kabudi pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kuwa mdau mkubwa wa sekta ya michezo hapa nchini kupitia jitihada zake mbalimbali, alisema ukubwa wa mashindano hayo ya NBC Dodoma Marathon unatoa fursa kwa mamlaka zinazosimamia mchezo huo kutumia washindi mbalimbali waliopatikana kwenye mbio hizo kuliwakilisha taifa kwenye mashindani mbalimbali ya kimataifa yakiwemo mashindano ya Olympics na yale ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth).

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi alisema kiasi cha mil 400 kati ya fedha zilikusanywa kupitia mbio hizo kitaelekezwa katika kufanikisha malengo ya mbio hizo ambayo ni kuendeleza mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, kupanua ufadhili wa wakunga hadi kufikia wakunga 200 pamoja na kuanzisha mpango mpya wa kufadhili masomo ya wauguzi 100 kwa ajili ya watoto wenye changamoto za usonji (autism) nchini.

Aidha Sabi pamoja na Dk. Biteko walikabidhi hundi za fedha zilizotokana na mbio hizo ambapo kiasi cha Tsh mil 200 kilikabidhiwa kwa taasisi ya Benjamini Mkapa ili kupanua ufadhili wa wakunga hadi kufikia wakunga 200, Fedha kiasi cha sh mil 100 kilikabidhiwa kwa taasisi ya Ocean Road ili kuendeleza mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kiasi cha mil 100 kilikabidhiwa kwa taasisi ya AMREF Health Africa kwa ajili ya watoto wenye changamoto za usonji (autism) nchini.

“Mafanikio haya yanachochewa na dhamira yetu kama benki ya kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii tunayoihudumia. Pia nawapongeza sana wadau mbalimbali waliojitokeza kufanikisha mbio hizo wakiwemo wadhamini wetu wakuu Kampuni ya GSM Group sambamba na wadhamini wengine muhimu ikiwemo Kampuni ya Bima ya Sanlam pamoja na wadhamini wengine wote waliotuunga mkono,’’ alisema.

About The Author

error: Content is protected !!