July 16, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yazitambulisha jezi za NBC Dodoma Marathon kwa wadau, Sanlam wapongeza ubora

 

MUANDAAJI wa mbio za NBC Dodoma Marathon, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeanza rasmi utambulisho wa jezi maalum na vifaa vitakazotumiwa na washiriki wa mbio hizo kwa kuzikabidhi kwa wadau mbalimbali wakiwemo wadhamini wa mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Julai 27, mwaka huu jijini Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Zoezi hilo liloanza leo jijini Dar es Salaam liliongozwa na Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Rayson Foya, likianzia kwa mmoja wa wadhamini muhimu mbio hizo Kampuni ya Bima ya Sanlam huku likitarajiwa kuendelea kwa wadau wengine wengi wakiwemo wadhamini, taasisi wanufaika wa mbio hizo, wadau wa mchezo huo pamoja na viongozi waandamizi wa serikali.

Hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa hivyo imefanyika leo makao makuu ya Kampuni ya Bima ya Sanlam jijini Dar es Salaam ambapo ilishuhudiwa, Foya alieambatana na baadhi ya maofisa wa benki hiyo akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa benki hiyo, Godwin Semunyu wakipokelewa na mwenyeji wao Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bima ya Sanlam, Julius Magabe sambamba na maofisa wengine waandamizi wa kampuni hiyo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Foya pamoja na kuishukuru kampuni ya Bima ya Sanlam kwa kuwa wadhamini muhimu wa mbio hizo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2020, alisisitiza kuhusu umuhimu na nafasi wa wadau hao katika kufanikisha kusudi la mbio hizo la kuendeleza mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, kupanua ufadhili wa wakunga hadi kufikia wakunga 200 pamoja na kuanzisha mpango mpya wa kufadhili masomo ya wauguzi 100 kwa ajili ya watoto wenye changamoto za usonji (autism) nchini.

“NBC Dodoma Marathon sio tu tukio la kimichezo bali pia ni jukwaa la matumaini ya maisha kwa watanzania. Ushiriki wa Sanlam kwenye mbio hizi kupitia udhamini wao umekuwa ni chachu muhimu katika kufanikisha kusudi leo hilo mihumu. Leo hii tunawakabidhi jezi hizi zenye mvuto na ubora wa hali ya juu wadau wetu wa Sanlam ikiwa namna ya kuheshimu mchango wao huo kipekee kabisa na tutaendelea na zoezi hili kwa wadau wetu wengine wengi ikiwa ni ishara ya sisi kutambua mchango wao kwetu kwa faida ya taifa letu,’’ alisema.

Kwa upande wake, Magabe pamoja na kupongeza ubora na ubunifu wa jezi hizo, aliishukuru benki hiyo kwa namna inavyoandaa tukio hilo kwa weledi wa hali ya juu hatua ambayo imeongeza mvuto wake kiasi cha kuwavutia maelfu ya washiriki kutoka ndani na nje ya nchi.

“Zaidi tunawapongeza NBC kwa namna ambavyo wamekuwa wakilitumia tukio hilo kukusanya fedha kwa ajili ya kufanikisha makusudi muhimu ya mbio hizi. Ni kupitia kuridhishwa kwetu na nia pamoja na uratibu wa mbio hizo ndio imekuwa sababu ya Sanlam Insurance kuendelea kuziunga mkono kama wadau muhimu tangu kuanzishwa kwake huu ukiwa ni msimu wake wa sita na tunaahidi kuendelea kuziunga mkono zaidi katika misimu mingine ijayo,’’ alisema.

Akizungumzia maandalizi ya mbio hizo, Semunyu alisema mwitikio wa washiriki kutoka ndani na nje ya nchi ni mkubwa huku usajili wa mbio hizi ukiendelea kupitia tovuti ya www.events.nbc.co.tz ambapo washiriki wanatakiwa kuchangia kiasi cha TZS 45,000 kwa usajili wa mtu mmoja mmoja au 42,000 kwa usajili wa kikundi chenye idadi ya watu 30 au zaidi.

About The Author

error: Content is protected !!