July 12, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Siamini ‘sana’ dhana ya uandishi wa katikati – Prof. Mkumbo

PROFESA Kitila Mkumbo anasema yeye haamini katika dhana ya mwandishi au chombo cha habari kutochukua upande linapotokea tukio linaloonesha wazi kuna dhulma. Anaripoti Jabir Idrissa, Dar es Salaam … (endelea).

Akihutubia wahariri kwenye mkutano na Tume ya Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, juzi jijini Dar es Salaam, Prof. Kitila alisema anatambua wajibu na mchango wa vyombo vya habari nchini na angependa viimarike ili kutekeleza jukumu lake la kijamii kwa ufanisi zaidi.

Amesema serikali inaona mchango mkubwa wa vyombo vya habari na kwamba inafikiria namna ya kuvisaidia uwezo wa kiutendaji kusudi viwe imara zaidi na kutumainiwa na umma, mbali na serikali yenyewe.

Prof. Kitila ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, alisema katika mkutano huo uliokutanisha karibu wahariri 100, penye tukio ni muhimu mwandishi wa habari akawa na imani kuwa yupo alodhulumiwa ambaye anastahili kutambuliwa na kuinuliwa sauti yake.

“Mwandishi ni kioo cha jamii. Anatakiwa kuwakilisha sauti za watu wanaoonewa. Unakosaje upande wakati unaona bayana huyu mtu hapa ameonewa, pengine na mwenye uwezo,” anahoji.

Lakini, akizungumzia maoni ya kwamba vyombo vya habari nchini haviko sawa kiuwajibikaji, Prof. Kitila alisema hiyo ni dharau isiyokubalika na kuhimiza waandishi kutokubali kudharauliwa.

Prof. Kitila Mkumbo

Alidiriki kuwaita “wapumbavu” watu wanaodharau na kubagaza waandishi na vyombo vya habari kwa kuwa vina mchango mkubwa ambao kwa serikali huutumia kujipima kimwenendo kutokana na namna inavyoonekana na vyombo vya habari.

Kwenye mkutano huo, Prof. Kitila aliandamana na watendaji wa Tume ya Mipango ya Taifa wakiongozwa na Katibu Mtendaji Dk. Fred Msemwa na Mjumbe wa Bodi ya Tume, Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, kuelezea kukamilika kwa uandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo Tanzania 2050 na kusema inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 17 Julai 2025.

Dira hiyo inayoonesha ni vipi Tanzania inatakiwa kuwa ifikapo mwaka 2050, kiuchumi, kijamii na kisiasa, imeandaliwa kupitia hatua 12, ya mwisho ikiwa ya kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano, mnamo tarehe 22 Juni, kabla ya kufungwa kwa kuhutubiwa na Rais Samia Juni 26.

Prof. Kitila amesema dira imeandaliwa kwa kuzingatia “makubaliano ya kitaifa” {National Consensus} kiasi cha kuamini kuwa imejumuisha maoni ya makundi mbalimbali nchini yakiwemo mawazo ya kiuchambuzi yaliyotokana na mifano ya dira ya maendeleo ya nchi nyengine zikiwemo za Afrika na Mashariki ya Mbali {Bara la Asia}.

Makundi yaliyofikiwa na kutoa maoni na mapendekezo ni wataalamu wa sekta tofauti, viongozi wa kitaifa wakiwemo wastaafu, wakurugenzi na watendaji wa mipango serikalini, waandishi wa habari, bila ya kusahau wawakilishi wa vyama vya siasa.

“Ndio maana ni msimamo wetu kutarajia ilani za vyama vya siasa kueleka uchaguzi mwaka huu zitakuwa zilizoandaliwa kwa kuzingatia mfungamano na Dira ya Taifa ya Maendeleo,” alisema.

Mbali na kutumia nyaraka mbalimbali, Prof. Kitila amesema dira iliangalia masuala kadhaa yanavyosimamiwa katika nchi za Botswana, Mauritius, Morocco, Afrika Kusini na Kenya; pamoja na mataifa yaliyoendelea – China, India, Indonesia, Singapore, Korea Kusini na Vietnam.

Rasimu ya kwanza ya Dira iliyopewa jina la kifupisho la Tanzania Tuitakayo 2050, ilizinduliwa Desemba mwaka jana, miaka miwili karibu tangu hatua ya kwanza ya maandalizi ilipoanza mwaka 2023. Hatua hiyo ya uzinduzi ilitanguliwa na kazi ya uchambuzi wa nyaraka na ripoti mbalimbali za kitaifa. Baada ya uzinduzi, rasimu ya awali ilipelekwa kwa wananchi na wadau walioitolea maoni na mapendekezo.

About The Author

error: Content is protected !!