June 30, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC ‘yawanoa’ wataalam teknolojia ya Huduma za Fedha ili kuchochea uchumi jumuishi

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imeendesha semina maalum kwa ajili ya wadau wa Umoja wa Makampuni yanayotoa Huduma za Kifedha kupitia Teknolojia Tanzania (TAFINA) ikilenga kuwajengea uwezo zaidi wadau hao ili waweze kubuni huduma mbalimbali zinazoendana na mahitaji halisi ya jamii na taasisi za kifedha hususani benki hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Zaidi kupitia mafunzo hayo benki hiyo ililenga kuwajengea uwezo wadau hao kuhusu namna bora na rahisi ya kuyafikia masoko pamoja na kunufaika kupitia uwezeshwaji wa mikopo ili kukuza jitihada zao katika kuchochea uchumi jumuishi kupitia huduma za kifedha zilizorahisishwa kupitia teknolojia.

Semina hiyo ya siku moja iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam ilihusisha wadau hao pamoja na maofisa na wataalamu wa teknolojia ya huduma za kifedha kutoka benki ya NBC ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano baina ya washirika hao wawili yaliyosainiwa mapema mwezi Aprili mwaka huu jijini humo.

Akizungumza wakati wa semina hiyo Mkuu wa Kitengo cha Miamala ya Kibenki kutoka Benki ya NBC, Mangire Kibanda alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za benki hiyo katika kuongeza kasi ya uakuaji wa teknolojia katika utoaji wa huduma za kifedha huku ikithibitisha dhamira yake ya kuwa benki kinara katika utoaji wa huduma za kibenki kwa njia ya kidijitali na ubunifu kuelekea mapinduzi makubwa ya utoaji wa huduma za kifedha.

“Kinachofanyika leo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano yetu na wadau wa TAFINA tuliyo saini nao mapema mwezi April mwaka huu. Kupitia semina hii tunalenga kuwajengea uwezo zaidi kupitia wataalam wetu na maofisa wa huduma zetu mbalimbali ili waweze kutambua huduma zetu za kibenki, ubora wake na nini tunahitaji zaidi ili kuendeleza ufanisi wetu kwa wateja, ili wao kama wataalamu wawe kwenye nafasi ya kuweza kubuni huduma zinazoendana na mahitaji halisi si tu kwa ajili yetu bali pia hata kwa taasisi nyingine zenye uhitaji wa huduma hizo,’’

Zaidi Kibanda alisema kupitia semina hiyo, pamoja na washirika hao kujadili namna ya kushirikiana kuunda na kutoa bidhaa maalum kama vile njia za malipo kidijitali (payment gateways), mikopo ya kidijitali, na huduma za kifedha zilizounganishwa (embedded finance solutions) pia walijadili namna bora ya kuwaimarisha na kuwawezesha kifedha wadau hao kupitia mikopo rafiki ili waweze kuboresha bunifu zao.

“Ni kupitia bunifu zilizowezeshwa na kuboreshwa zaidi ndio wadau hawa wataweza kuja na bidhaa bora na zenye uwezo wa kuchochea ujumuishi wa kifedha kwa Watanzania wote kwa kuhakikisha kuwa huduma za kifedha zinapatikana kwa urahisi, kwa gharama nafuu, na kwa ufanisi zaidi,’’ aliongeza.

Kwa upande wake Meneja Mahusiano na Ushirikiano wa Wadau wa TAFINA, Julieth Kiluwa pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa ushirikiano inaoendelea kuuonesha kwa wadau hao alisema kupitia semina hiyo wadau wameweza kujijengea uwezo zaidi katika kutambua huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa na taasisi hiyo hatua ambayo kwa kiasi kikubwa itawasaidia kujua namna bora ya kubuni huduma zinazolenga kuboresha na kurahisisha zaidi huduma hizo kwa manufaa ya taasisi na wateja kwa ujumla.

“Kupitia ushirikiano huu tunashukuru kwa niaba ya wanachama wetu kuona kwamba tuna mshirika mwenye nguvu ambae anaendelea kutushika mkono kuelekea ndoto zetu za kurahisisha utoaji wa huduma za kifedha kupitia teknolojia. Mbali na mafunzo haya tunaamini kupitia mikopo ya NBC yenye upendeleo kwa wanachama wetu itasaidia ukuaji wa kampuni nyingi za kibunifu huku pia tukipata fursa ya kuwa benki mlezi iliyo karibu zaidi na sisi kwenye vumbuzi zetu zinazolenga kurahisisha utoaji wa huduma za kifedha kupitia teknolojia,’’ alisema.

About The Author

error: Content is protected !!