June 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Madiwani Malinyi kifua mbele, waitendea haki serikali

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba

 

MKUU wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, Sebastian Waryuba amesema, madiwani na wadau wa maendeleo wa wilaya hiyo, wameitendea haki serikali katika kipindi cha miaka mitano (2020 – 2025). Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).

Akizungumza wakati wa Kikao cha Wadau wa Maendeleo Malinyi kilichoandaliwa na halmashauri ya wilaya hiyo tarehe 19 Juni 2025, DC Waryuba alisema, hatua ya halmashauri hiyo kupandisha mapato yake kutoka Tsh. 2.2 Bilioni (2020/21) mpaka Tsh. 4.5 Bilioni (2024/25) kimerahisisha kazi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Malinyi.

“Madiwani mnamaliza awamu hii kifua mbele, kiwango cha mapato wakati mnaingia na mnapotoka kinathibitisha hilo. Mliingia mapato yakiwa Tsh. 2.2 Bil mwaka 2021 na mnatoka mapato yakiwa Tsh. 4.5 Bil 2025. Huduma nyingi zimeboreshwa.

“Mmepata bahati ya kumaliza na mkurugenzi huyu ambaye utendaji wake umeleta mwanga zaidi, kwa mwaka 2024/25 tu kaongeza mapato kwa zaidi ya Tsh. 1 Bilioni,” alisema DC Mwaryuba.

Akitoa ripoti ya mwenendo wa halmashauri hiyo kwa miaka mitano (2020 – 2025), mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Khamis Katimba alisema awali halmashauri hiyo ilikuwa ikiongeza mapato yake kwa wastani wa Tsh. 200 – 300 Milioni kila mwaka.

“Lakini zaidi kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 halmashauri hiyo imeongeza mapato yake kwa zaidi ya Tsh. 1 Bilion. Mapato ya Mwaka 2023/24 yalikuwa Tsh 3. 5 Bilion na 204/25 ni Tsh. 4.5 Bilioni, na hii ingeongezeka zaidi ya Tsh. 200 Milion ila mvua imeathiri pakubwa,” alisema mkurugenzi huyo.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Malinyi, Saida Mhanga alisema, ripoti ya mkurugenzi imetoa picha halisi ya namna halmashauri hiyo ilipotoka na ilipo sasa.

“Tunashukuru mkurugenzi, hatukuwahi kufikia kiwango kikubwa cha makusanyo kwa namna hii katika miaka ya nyuma, hili tunajivunia. Wilaya yetu ina mafanikio makubwa, madiwani mjiamini kazi mmeifanya,” alisema.

Kwenye kikao hicho, makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jenny Komba alisema “tunamaliza ngwe hii lakini leo niseme, sisi kama madiwani wa wilaya hii, tunamaliza tukiwa na amani. Tunacho cha kuwaeleza wananchi wetu kuhusu shuhuli za maendeleo chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.”

Maina Mrisho, mdau wa maendeleo Malinyi aliwaomba wananchi wenzake kwenye kikao hicho kwa pamoja kumpongeza mkurugenzi na madiwani kwa kufanya kazi kwa weledi.

“Sisi tunamsifu kwa kuwa anakusanya na anafanya jambo ambalo wote tunameona, kwa mfano hatukuwa na huduma ya jengo la kuhifadhia maiti, lakini ndani ya miezi yake 10 jengo limesimama na sasa linafanya kazi,” alisema.

Shaibu Omari, Katibu wa Chama cha Walimu Wilaya ya Malinyi alimkumbusha mkurugenzi kuendelea kutoa stahili za walimu.

About The Author

error: Content is protected !!