June 16, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC, Mbogo Ranches zasaini makubaliano ya Utoaji Mikopo ya Mbegu Bora ya Mifugo kwa Wafugaji

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesaini makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Mbogo Ranches yanayotoa fursa kwa wafugaji nchini kuweza kunufaika kupitia upatikanaji wa mikopo rafiki kutoka benki hiyo kwa ajili ya ununuzi wa mbegu bora za kisasa za mifugo ikiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo inayozalishwa na kampuni hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).

Hatua hiyo inalenga kuwasaidia kwa kiasi kikubwa wafugaji nchini ambao wamekuwa wakishindwa kumudu gharama kubwa za ununuzi mbegu hizo.

Hafla fupi ya kusaini makubaliano hayo imefanyika leo kwenye Maonesho ya Mifugo ya Kimataifa ya Mbogo 2025 yaliyofanyika kwa siku mbili katika Viwanja vya Maonesho vya Ubena Zomozi, Chalinze mkoani Pwani.

Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na Wakubwa wa benki ya NBC, Elibariki Masuke alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw Theobald Sabi kwenye tukio hilo huku upande wa kampuni ya Mbogo Ranches ikiwakilishwa na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Naweed Mulla.

Akizungumzia hatua hiyo Masuke alisema ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo katika kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta ya ufugaji na kilimo nchini kupitia uchumi jumuishi unaochagizwa na huduma rasmi za kifedha.

“Kupitia makubaliano haya wafugaji kote nchini watakaotembelea mashamba ya Mbogo Ranches na kuvutiwa na mbegu ya aina yoyote iwe ya ng’ombe, mbuzi au kondoo wanayo fursa ya kuwasiliana na tawi lolote la benki ya NBC na tutawawezesha kukopa mbegu hiyo kwa makubaliano ya wao kutulipa sisi kidogo kidogo kwa bei ile ile ya shambani,’’ alifafanua Masuke.

Kwa mujibu wa Masuke, hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itasaidia kuleta mapinduzi kwenye sekta ya mifugo nchini kutokana na urahisishwa mkubwa wa upatikanaji wa mbegu bora na za kisasa za mifugo ya aina mbalimbali.

Kwa upande wake Mulla, pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa hatua hiyo muhimu alisema mikopo hiyo itawasaidia kwa kiasi kikubwa wafugaji nchini ambao wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za kununua mbegu hizo zinazouzwa kwa bei ya juu kutokana na gharama kubwa ya matunzo na usafiri kutoka nje ya nchi.

“Pamoja na uwekezaji wetu huu kwenye mbegu bora za kisasa za mifugo, bado wafugaji wengi nchini hawana uwezo wa kumudu gharama za kununua mbegu hizi na hivyo wamekuwa wakibaki kutumia mbegu za asili ambazo nyingi haziwasaidii kupata uzalishaji wa kutosha. Hivyo kupitia makubaliano haya ambayo ni kwanza kwetu wafugaji wengi wataweza kupata mikopo itakayowasaidi kumudu gharama hizi na hivyo kuweza kumiliki mbegu bora za mifugo. Tunawashukuru sana NBC kwa kutushika mkono kwenye hili,’’ alisema Mulla.

Aidha Mulla alitoa wito kwa wafugaji nchini kugeukia ufugaji wa kisasa hatua ambayo inakwenda sambamba na urasimishaji wa shughuli zao za ufugaji kupitia usajili rasmi, ufunguaji wa akaunti rasmi za kibenki pamoja na kumiliki namba za mlipa kodi (TIN Number) ili kuwarahisishia michakato ya kiuendeshaji ikiwemo mikopo na fursa nyingine zinazohitaji utambuzi urasmi.

“Fursa kama hizi zinakuja kwa wafugaji ambao wapo tayari kuzipokea na hilo linawezekana tu pale wanapokuwa wameweza kurasimisha shughuli zao’’ aliongeza.

Hafla hiyo pia ilihusisha uwepo wa wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo nchini wakiwemo wafugaji pamoja na maofisa wengine waandamizi wa benki ya NBC wakiwemo Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo na wakulima kutoka Benki ya NBC, Raymond Urassa na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki hiyo Bw David Raymond.

Akielezea namna ya kunufaika na mpango huo Urassa aliwaomba wafugaji kufungua akaunti ya Mfugaji ya benki ya NBC ambayo ni mahususi kwa kundi hilo ikiwa haina makato yotote ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.

About The Author

error: Content is protected !!