June 15, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Vifungu vilivyozuia kushtakiwa Rais, Spika, Jaji Mkuu, Waziri Mkuu vyabatilishwa

 

MAHAKAMA ya Rufaa ya Tanzania leo imeagiza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuta vifungu vinne vya sheria vilivyokuwa vikiweka vikwazo mashauri ya kikatiba yenye maslahi ya umma. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Mwaka 2020 bunge lilifanya merekebisho ya sheria mbalimbali pamoja na zile utekelezaji wa Haki za msingi na wajibu (sura ya 3) kwa kuongeza vifungu vya 4(2), 4(3), 4(4), na 4(5).

Vifungu hivyo ni mwiba kwa mashauri yenye maslahi ya umma ambayo vilikuwa vilazimisha muambajio awe na muathirika wa moja kwa moja na jambo liliomfanya afungue shauri pia mashauri yote yanayowahusu viongozi wakuu kama vile Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika wa Bunge na Jaji Mkuu, yafunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu na sio kuwahusisha viongozi hao.

Uamuzi huo umesomwa jana tarehe 23 Juni 2025, na Joseph Fovo, Naibu Msajili wa mahakama hiyo ambaye aliusoma kwa njia ya mtandao.

Uamuzi huo uliobatilisha vifungo vyote vinne vilivyolalamikiwa aliyefungua shauri hilo Wakili Onesmo Olengurumwa, mwanaharakati wa haki za binadamu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Rufaa hiyo Na. 134 ya Mwaka 2022 iliyosikiliza mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa: Jaji Rehema Levira, Jaji Wilfred Rumanyika na Jaji Gerald Ngwembe. Wakili Olengurumwa aliwakilishwa na jopo la mawakili maarufu likiongozwa na Prof. Issa Shivji pamoja na Dk. Rugemeleza Nshala, Mpale Mpoki na Wakili John Seka.

Uamuzi huo ulisema kuwa:- Kifungu cha 4(2) kinavunja dhana ya mashauri ya maslahi kwa umma kwa kuhitaji waathirika binafsi pekee, hali inayokinzana na Ibara ya 26(2) ya Katiba.

Kifungu cha 4(3) ni batili kwa kuwa kinachanganya masharti ya Ibara ya 30(3) (maslahi binafsi) na haki za maslahi kwa umma zinazolindwa chini ya Ibara ya 26(2).

Kifungu cha 4(4) ni batili kwa kuwa Mwanasheria Mkuu hana mamlaka ya kikatiba kuwakilisha mihimili mingine, hasa Mahakama au viongozi wa kisiasa walio huru kikatiba kama Jaji Mkuu.

Kifungu cha 4(5) pia ni batili kwa kuwa hakuna sheria nyingine zinazotoa nafuu ya moja kwa moja kwa mashauri ya maslahi ya umma.

KIlicholalamikiwa awali

Kifungu cha 4(2): Kilihitaji mtu anayetaka kufungua kesi ya kikatiba kuambatanisha kiapo kinachoeleza namna alivyoathirika binafsi na ukiukwaji huo.

Kifungu cha 4(3): Kiliongeza kizuizi kwa mashauri ya maslahi ya umma kwa kutaka mlalamikaji aonyeshe maslahi binafsi sawa na Ibara ya 30(3) ya Katiba.

Kifungu cha 4(4): Kiliweka sharti kuwa kesi dhidi ya viongozi waandamizi serikalini – Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika na Jaji Mkuu – zifunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali badala ya wahusika hao moja kwa moja.

Kifungu cha 4(5): Kilimtaka mtu anayepanga kufungua kesi kutafuta kwanza nafuu kupitia sheria nyingine zilizopo kabla ya kufungua kesi chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi.

Awali, Mahakama Kuu ya Tanzania iliitupilia mbali kesi hiyo mnamo Februari 15, 2022, kwa maelezo kuwa vifungu hivyo havivunji Katiba wala mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu. Mahakama Kuu ilisisitiza kuwa vifungu hivyo vinakamilisha Ibara ya 26(2) na 30(3) ya Katiba, na vinaakisi misingi ya utawala wa sheria, mgawanyo wa madaraka, na mfumo wa kimataifa wa haki.

Hata hivyo, Wakili Olengurumwa hakuridhika na uamuzi huo na kukata rufaa Mahakama ya Rufaa mwaka huo huo wa 2022.

Profesa Issa Shivji, Mwanazuoni mkongwe nchini Tanzania ambaye pia ni mmoja wa mawakili waliomwakilisha Olengurumwa kwenye shauri hilo amesema kuwa uamuzi huo ni umetoa faraja kwenye duru za haki “ni uamuzi wa kijasiri imepita takibani miaka 10 mahakama haijawahi kufanya uamuzi kama huu.”

About The Author

error: Content is protected !!