June 12, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yakabidhi gawio la Sh. 10.5 bilioni kwa Serikali, Msajili Hazina apongeza

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi kiasi cha Sh. 10.5 bilioni kwa Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni gawio kwa Serikali kwa mwaka 2024. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamiliki asilimia 30 ya hisa za Benki ya NBC, hivyo kunufaika moja kwa moja na gawio hilo ambalo limetokana na faida iliyopatikana mwaka 2024. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua hiyo ya benki ya NBC inafuatia mafanikio ya kiuendeshaji na kiutendaji kwa mwaka 2023/2024 ambapo benki hiyo ilitangaza jumla ya gawio la Shilingi za Tanzania bilioni 35 kwa wanahisa wake kufuatia faida ya kabla ya kodi ya shilingi bilioni 170.

Gawio hilo limetolewa jana Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kitaifa ya kupokea gawio na michango kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma pamoja na kampuni ambazo serikali inamiliki hisa. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali waandamizi wa serikali na taasisi mbalimbali akiwemo Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu.

Benki ya NBC iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Dk. Elirehema Doriye, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji, Theobald Sabi.

Katika hafla hiyo Rais Samia alitoa wito kwa Mashirika na Taasisi za Umma kuhakikisha yanawajibika ipasavyo katika kulinda na kuendeleza uwekezaji wa Serikali kwenye mashirika hayo, na kuchangia kikamilifu kwenye maendeleo ya kiuchumi.

Akizungumzia hatua ya benki ya NBC, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, aliipongeza benki ya hiyo kwa utendaji mzuri huku akiitaja benki hiyo kama moja ya taasisi zenye hisa chache za serikali ambazo zinazojiendesha kwa ufanisi huku zikiwa na muendelezo wa utoaji wa gawio usiotetereka.

“Serikali kwa sasa ina umiliki wa asilimia 30 kwenye Benki ya NBC, na tumeshuhudia gawio likipanda kwa asilimia 600 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Tunajivunia kuona kwamba leo tunapata jumla ya shilingi za Tanzania bilioni 10.5 kama gawio kwa mwaka uliopita. Haya ni mafanikio yanayostahili kupongezwa na yanayoashiria mabadiliko makubwa katika utendaji na uendeshwaji wa benki hii,” alisema Mchechu.

“Ninawatakia heri bodi ya wakurugenzi na timu ya usimamizi na uendeshaji wa benki kwa mafanikio haya huku nikiwaasa waendeleze mwenendo huu chanya kwa manufaa ya wadau wote,” aliongeza.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema hatua hiyo ni uthibitisho wa mkakati mzuri wa ukuaji na mabadiliko wa benki hiyo sambamba na utendaji thabiti katika soko.

“Kama benki tumedhamiria kutoa huduma mbalimbali za benki, kuanzia huduma binafsi za benki na huduma za kibenki kwa ajili ya biashara na hivyo kuwa suluhisho muhimu kiuchumi kupitia huduma zetu mbalimbali zinazopatikana kupitia mtandao mpana wa matawi yetu yaliyoenea kimkakati katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mawakala wetu na njia za kisasa za kidijitali.’’ Alisema Sabi.

Mbali na umiliki wa asilimia 30 wa serikali kwenye benki ya NBC, benki hiyo yenye umri zaidi ya miaka 58, pia inamilikiwa kwa asilimia 55 na Absa Group Limited ya Afrika Kusini huku asilimia 15 zikimilikiwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC).

About The Author

error: Content is protected !!