May 31, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC  yakabidhi Kombe la Ubingwa wa Vijana (U20) kwa Azam FC

 

MDHAMINI Mkuu wa Ligi ya NBC Vijana chini ya miaka 20 (NBC U20 Youth League) Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi kombe la ubingwa wa ligi hiyo kwa timu ya Azam FC (U20) ya jijini Dar es Salaam baada ya timu hiyo kuibuka bingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa 2024/2025 kufuatia ushindi wake wa goli 1 – 0 dhidi ya wenzao Foutain Gate (U20). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Shujaa wa Azam FC (U20) jana alikuwa ni mshambuliaji Carlos Chasambi aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 11 ya mchezo.

Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa huo ilifanyika jana katika uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es Salaam. Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Biashara benki ya NBC ambae ndio Mwenyekiti wa kamati ya Ligi Kuu ya NBC ndani ya benki hiyo, Joseph Lyuba aliwaongoza wafanyakazi wengine wa benki hiyo kwenye tukio hilo lililopambwa na uwepo wa mashabiki na wadau mbalimbali wa mchezo huo wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoani Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Lyuba alivipongeza vilabu shiriki vya ligi hiyo hususani mshindi timu ya Azam FC (U 20), mshindi wa pili Fountain Gate FC (U20), mabenchi ya ufundi pamoja na TFF huku akielezea namna ambavyo ushindani kwenye ligi hiyo umeboreka, hatua ambayo kwa mujibu wake inathibitisha muelekeo mzuri katika ukuaji wa mchezo wa soka hapa nchini.

“Msukumo wa NBC kudhamini ligi hii ya vijana unachagizwa na dhamira yetu ya kuwa na ligi kuu yenye ubora na ushindani kutokana na vipaji vinavyozalishwa hapa nchini. Tunaamini ili tuwe na Ligi Kuu ya NBC yenye mvuto na ushindani lazima tuanzie katika ngazi hii ya kuibua vipaji. Tunashuru kuona hili linaenda vizuri na matunda yake yataonekana zaidi kwenye ligi za NBC Championship, ligi Kuu ya NBC na hata timu ya Taifa,’’ alisema Lyuba.

Kwa mujibu wa Lyuba, Benki hiyo imejipanga zaidi kuendelea kuboresha udhamini wake kwenye ligi zote tatu inazozidhamini ili kuongeza kasi ya ushindani, kuboresha hadhi ya ligi hiyo, kuchochea ajira pamoja na kuboresha hali ya maisha ya wadau mbalimbali waliopo kwenye mnyororo wa mchezo huo ikiwemo wachezaji na mabenchi ya ufundi.

Akizungumzia mashindano hayo, Kocha Mkuu wa Azam FC (U20), Kassim Liogope pamoja na kuwapongeza wachezaji wake, uongozi wa timu hiyo, TFF na mdhamini benki ya NBC, alisema mashindano hayo yaliambatana na ushindani mkubwa hususani katika hatua ya nane bora kutokana na timu shiriki kubadilika kiuchezaji hatua ambayo inathibitisha uborekaji mkubwa wa viwango vya ubora wa vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo.

About The Author

error: Content is protected !!