June 1, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Madereva mkoani Songwe wasiofuata sheria wapewa onyo kali

 

MADEREVA wanaosafirisha abiria na mizigo kwenda sehemu mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Songwe wametakiwa kufuata sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za madereva wenzao wazembe ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Anaripoti Issa Mwadangala, Songwe … (endelea).

Hayo yamesemwa Mei 29, 2025 na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Charles Bukombe baada ya kufanya oparesheni ya ukaguzi wa magari ya abiria na mizigo katika Kituo cha Ukaguzi wa Magari Mkoani humo eneo la  Chimbuya Wilaya ya Mbozi.

SSP Bukombe alisema kuwa lengo la operesheni hiyo pamoja na ukaguzi huo ni kuangalia ubovu wa magari hasa ukaguzi wa mataili, kukagua madeni ya magari ambayo bado hayajalipwa, ukaguzi wa leseni, ujazaji wa abria kupita uwezo wa chombo ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa tiketi mtandao ili kuweza kuepusha ajali zinazoweza kuepukika ndani ya Mkoa wa Songwe.

“Niwaombe madereva na abiria mnatakiwa kutofumbia macho vitendo vya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani na badala yake mnatakiwa kukemea vitendo hivyo na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa,” alisema SSP Bukombe.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Mbozi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Anton Sabasaba alisema kuwa ameendelea kutoa elimu kwa abiria juu ya umuhimu wa kufichua taarifa za madereva wazembe ambao hawafuati sheria za usalama barabarani kama sheria na taratibu za usafirishaji abiria zinavyoelekeza ili waweze kufika salama waendapo.

Jeshi la Polisi nchini linaendelea na operesheni za ukaguzi wa vyombo vya moto ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya usalama barabarani ili kutokomeza ajali za barabarani hasa kwa watumiaji wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu kwa lengo la kupunguza ajali ambazo zinaepukika.

Katika Operesheni hiyo jumla ya magari 54 yalikaguliwa na magari 8 yalikutwa na changamoto ambazo zinaweza kusababisha ajali ikiwa ni pamoja na kukuta changamoto mbalimbali katika leseni 17 za madereva hao.

About The Author

error: Content is protected !!