
KASSIM Majaliwa waziri mkuu amekutana na Ishiba Shigeru Waziri Mkuu wa Japan, ambaye amemuhakikishia kuwa nchi hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania jambo ambalo linalenga kuchochea ukuaji wa uchumi kutokana na fursa zitakazoendelea kupatikana kupitia mahusiano hayo. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).
Amekutana na kiongozi huyo Mei 29, 2025 katika ofisi ya Waziri Mkuu Tokyo, Japan, ambapo Majaliwa amesema ahadi hiyo inazidi kutoa fursa ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan pamoja na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Majaliwa ametumia fursa hiyo kumueleza Waziri Mkuu huyo kuwa pamoja na miradi mingine wanayotekeleza nchini, Japan kupitia JICA iangalie uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuzifanyia ukarabati mkubwa barabara za Morogoro-Dodoma na barabara ya Kibiti-Lindi ambayo imeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
Amesema Waziri Mkuu wa Japan baada ya kupata maelezo hayo ameuelekeza uongozi wa JICA pamoja na Youichi Mikami Balozi wa Japan nchini Tanzania kwenda kutembelea barabara hizo na kuzifanyia tathmini ya uharibifu na kisha kuwasilisha taarifa ili Serikali ya Japan ione namna itakavyoshirikiana na Tanzania katika utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan amepongeza kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Japan na kwamba ameahidi kuhakikisha makampuni mbalimbali ya Japan yataendelea kufanyakazi na Tanzania ili kuisaidia katika kukuza uchumi, kuendelea masuala ya kijamii na teknolojia kwani wanatambua idadi ya watu nchini inaendelea kuongezeka.
ZINAZOFANANA
Kapinga ataja vigezo vya ziada upelekaji umeme vitongojini
Mradi wa PURE Growth Fund wafungua maombi na mapendekezo ya Nishati Safi na Biashara za Kilimo
Mpina ashangaa watu wanatekwa Waziri bado yupo ofisini