
RAIS Samia Suluhu Hassan amewaonya makada wa chama hicho wanataka kukipasua chama hicho wakae chini wajifikirie upya. Anaripoti Salehe Mohamed, Dodoma … (endelea).
Rais Samia amesema kwa maendeleo yaliyopo sasa na mipango ya baadae itakayokifanya kiwe imara zaidi yoyote mwenye nia ya kukipasua akafanye ‘home work’ yake tena.
Kauli hiyo ameitoa leo, tarehe 29 Mei 2025, katika Mkutano Mkuu, wakati akielezea namna jengo la CCM linaloanza kujengwa hivi sasa litakavyokuwa.
Licha ya Rais Samia kutoeleza kwa undani hoja ya kukipasua chama, hivi karibuni kumekuwa na minyukano miongoni mwa makada na viongozi wake juu ya uendeshaji wa serikali na matukio mbalimbali yanayotokea nchini.
“Jamani mnaona ramani ya jengo letu ilivyo nzuri na inavyonyesha thamani yetu, sasa tufanye maendeleo yanayoenda na umri wetu ambapo mwaka 2027 tutafikisha miaka 50 tangu tuzaliwe.
“Tunaondelea na harakati za kukipasua chama tujitathmini sisi ili tufikie malengo tuliyojiwekea tukiwa wamoja. Sasa wale wenye nia ya kukipasua chama watafakari upya,” amesema
Rais Samia amesema jengo hilo litakalokuwa na ghorofa tano litagharimu Sh. 34 bilioni mpaka kukamilika kwake linategemea nguvu na ushirikiano wa wanachama wote.
Rais Samia amesema mpaka sasa chama hicho kina wanachama 13 milioni hivyo anatarajia kasi ya kusajili wanachama itaongezeka.
Katika hatua nyingine wanachama wa CCM wamepitisha marekebisho ya katiba yanayotoa fursa kwa chama hicho kufanya baadhi ya vikao kwa njia ya kidijitali.
Jambo jingine walilopitisha ni kuongeza idadi ya wadhamini kutoka wanane wa sasa hadi tisa.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wamepitisha pia kipengele kinachozilazimisha kamati za siasa za mikoa na wilaya zisianzishe miradi ya kiuchumi bila ridhaa ya maandishi kutoka Baraza la Wadhamini wa chama hicho.
Kwa mujibu wa Rais Samia sheria ya usajili wa vyama vya siasa inataka idadi ya baraza la wadhamini isigawanyike kwa mbili.
ZINAZOFANANA
Kilatu: Msajili wa vyama anaupendeleo
Dk. Mwinyi ampa heko Rais Samia ujenzi wa ofisi mpya ya CCM
Msajili awakomalia kina Mnyika, Lema na wenzake