May 30, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kapinga ataja vigezo vya ziada upelekaji umeme vitongojini

JUDITH Kapinga Naibu Waziri wa Nishati,  amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi ya umeme katika Vitongoji kwa kuzingatia vigezo vya ziada ikiwemo ukubwa wa vitongoji, ukubwa wa Jimbo pamoja na mahitaji ya kiuchumi na kijamii. Anaripoti Joyce Ndeki, Dodoma … (endelea).

Lengo la kuweka vigezo hivyo ni kuhakikisha kuwa kila jimbo linakuwa na vitongoji vingi vilivyofikiwa na nishati ya umeme.

Kapinga ameyasema hayo leo Mei 29, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Christopher Olesendeka, Mbunge wa Simanjiro, aliyeuliza kwamba  Serikali imejipangaje kutekeleza miradi ya Vitongoji kulingana na jiografia ya Wilaya ya Simanjiro ambapo umbali kutoka Kitongoji kimoja hadi kingine ni zaidi ya kilometa kumi.

“Naibu Spika, tunatekeleza miradi hii ya Vitongoji kwa kuzingatia vigezo vya ziada, tumeangalia ukubwa wa jimbo husika, ukubwa wa Vitongoji na mahitaji ya kiuchumi na kijamii katika jimbo husika. Niwahakikishie Wabunge mtaona utofauti katika miradi hii tunayoitekeleza hivi sasa,”  amesema  Kapinga

Akijibu swali la Stella Manyanya Mbunge wa Nyasa  aliyeuliza kuhusu kitongoji cha  Songea Pori kilichopo katika Kijiji cha Lunyele  na Kitongoji cha Nindi kilichopo Kijiji cha Konganywita kufikishiwa nishati ya umeme, Kapinga amesema Vitongoji hivyo vimefanyiwa upembuzi yakinifu na kubainika vinahitaji njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kati kwa umbali wa kilometa tatu.

Amesema  Serikali inatarajia kuvipelekea umeme vitongoji hivyo kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B  (HEP IIB) ambao utekelezaji wake utaanza mwaka wa fedha 2025/2026.

Kuhusiana na kasi ndogo ya Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme katika Jimbo la Nyasa Kapinga amesema tayari Serikali imeshakutana na Mkandarasa na kumuagiza kuweka Wakandarasi wadogo (sub contractors) katika miradi yake anayotekeleza.

Akijibu swali la Aida Khenani Mbunge wa Nkasi Kaskazini, aliyetaka  kauli ya Serikali kuhusu kusuasua kwa Mkandarasi ambaye amepewa kazi ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji vilivyozunguka ziwa Tanganyika, Kapinga amesema katika utekelezaji wa miradi ya Vitongoji Serikali imehakikisha inawapata wakandarasi wenye weledi.

Kuhusu Wakandarasi ambao wanasuasua, Kapinga kwa niaba ya Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza mradi huo wa umeme kwenye Vitongoji vilivyozunguka ziwa Tanganyika.

Aidha, amemuagiza kuchukua hatua za ziada kwa Mkandarasi huyo kuhakikisha anatekeleza mradi huo kwa haraka na kwa weledi.

About The Author

error: Content is protected !!