
Waziri wa Madini, Antony Mavunde
WAZIRI wa Madini, Antony Mavunde, amesema wako kwenye mazungumzo na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya kuwezesha dhahabu kutumika kununua au kubadilishana bidhaa zinazohitajika hapa nchini. Anaripoti Salehe Mohamed, Dar es Salaam … (endelea).
Mavunde ametoa kauli hiyom leo tarehe 24 Mei, 2025 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) juu ya mafanikio yaliyopatikana wizarani kwake katika miaka minne ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema anaamini kwa njia hiyo si tu wataongeza mauzo ya dhahabu lakini itasaidia kulinda fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa mbalimbali nje ya nchi.
Mavunde anasema madini ya dhahabu ndiyo yanayouzwa kwa wingi kuliko mengine yaliyopo hapa nchini hivyo wanataka kuyatumia kwa ajili kuinufaisha Tanzania.
Amesema kuanzia mwaka jana BoT, walianza kuweka akiba ya dhahabu ambapo katika kipindi cha miezi minane wamefanikiwa kuwa na tani 3.7 na hivyo kuingia katika orodha ya nchi 10 za Afrika zenye akiba kubwa ya dhahabu.
“Tunataka tuitumike kikamilifu dhahabu yetu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu, tunataka ufike wakati badala ya kununua mafuta kwa fedha za kigeni tuwe tunayanunua kwa kutumia dhahabu. Tunanunua mafuta kwa wingi na tunatumia fedha nyingi za kununua bidhaa hiyo, tunaweza kubadilishana na wenzetu wanaohitaji dhahabu kwa bidhaa yoyote tunayoitaka”
“Rais Samia katuwekea mazingira mazuri ya kuhakikisha Watanzania tunanufaika na rasilimali tulizonazo, kazi yangu na watalaamu nilionao ni kuhakikisha ndoto ya maisha bora kwa Watanzania inafikiwa kwa njia iliyo bora kabisa” alisema
Waziri Mavunde amesema pia wako kwenye mkakati wa kuishawishi BoT ili kuanzisha utaratibu wa ununuzi wa sarafu za dhahabu kwa lengo la kuchochea upatikanaji wa fedha zaidi.
Amesema Rais Samia amefanya mabadiliko makubwa kwenye sekta ya madini ambapo wachimbaji wadogo wamekuwa wakisaidiwa utaalamu, mitaji na maeneo ya kufanyia kazi.
Mavunde amesema wamefuta leseni za watu waliohodhi maeneo bila ya kuyaendeleza na wako kwenye maandalizi ya kuyagawa kwa wachimbaji wadogo wenye uhitaji.
“Tumejiwekea lengo ifikapo mwaka 2030 tuwe tumepima asilimia 50 ya ardhi yetu ili iwe rahisi kujua eneo gani yanapatikana madini na ya aina gani. Tukifikia lengo hili nina hakika sekta ya madini itachangia zaidi ya asilimia 16 ya sasa katika pato la Taifa” amesema.
Amesema miongoni mwa mafanikio ya miaka minne ni kuliwezesha Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuwekeza katika sekta ya madini ikiwemo kulitengea Sh 7 bilioni kwa ajili ya utafiti wa maeneo yenye madini.
“Tunataka Stamico akafanye uwekezaji mkubwa kwa kufanya utafiti na baadae kumiliki migodi mikubwa. Tunataka shirika hili lifanane na kampuni nyingine zinazofanya biashara ya madini.”
“Tunakwenda kufungua kampuni mpya itakayopewa jukumu la kuendesha migodi ya Stamico kwa ufanisi zaidi. Tumedhamiria kuongeza thamani madini. Ninaamini huku tuendako tutakuwa na mafanikio zaidi” amesema.
Naye Mjumbe wa Kamati Tendaji ya TEF, Salim Said Salim, ameitaka Serikali kuwa na utaratibu wa kupeleka watalaamu wake nje ya nchi kwenda kujifunza masuala mbalimbali na kuweka mikakati imara ya kusimamia utekelezaji wa kile walichojifunza.
ZINAZOFANANA
Meridianbet yachochea mapinduzi ya kijani Kimya kimya: Miradi 80 ya Uendelevu Yatekelezwa Katika Robo ya Kwanza ya 2025
Mchengerwa aagiza maofisa Habari kukabidhiwa ofisi, awaonya MA-DED
Chaumma watangaza oparesheni ya C4C, kurusha chopa nchi nzima