
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi msimu wa sita wa mbio za NBC Dodoma Marathon zinazotarajiwa kufanyika Julai 27 mwaka huu jijijni Dodoma. Katika msimu wa mwaka huu benki hiyo inatarajia kuvunja rekodi ya ushiriki kwa kufikisha wakimbiaji 12,000 kutoka wakimbiaji 8,000 msimu uliopita na hivyo kuiweka kama moja ya mbio kubwa zaidi nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Rayson Foya, katika msimu huu mbio hizo zinalenga kukusanya fedha kiasi cha Sh. 700 milioni, ambazo zitasaidia kuendeleza mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, kupanua ufadhili wa wakunga hadi kufikia wakunga 200 pamoja na kuanzisha mpango mpya wa kufadhili masomo ya wauguzi 100 kwa ajili ya watoto wenye changamoto za usonji (autism) nchini.
Hafla ya uzinduzi wa mbio hizo imefanyika leo jijini Dar es Salaam ikihusisha wadau mbalimbali wa mbio hizo zikiwemo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Taasisi ya Benjamin Mkapa na Amref Health Africa ambazo ni wanufaika wa mbio hizo, wadhamini pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo wakiongozwa na Foya aliemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Foya alisema kuelekea msimu wa sita wa mbio hizo zitakazohusisha mbio za KM 5, KM 10, Nusu-Marathon (KM 21) na Marathon Kamili (KM 42), benki hiyo inajivunia mafanikio makubwa ya mbio katika kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake ikiwemo kukusanya zaidi ya shilingi Billion 1, ambapo zaidi asilimia 80 ya fedha hizo zimeelekezwa katika mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
“Aidha, tumefanikiwa kuwafikia zaidi ya wanawake takribani 200,000 ambapo zaidi ya wanawake 3,000 kati yao wanapatiwa matibabu, na wanawake 80 wameripotiwa kupona kabisa na kurejea kwa familia zao. Zaidi, tumetoa ufadhili kwa wakunga 100 kwa kushirikiana na taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation ili kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi (maternal mortarity). Mwaka huu tunatarajia kupanua wigo huu hadi kufikia wakunga 200.’’ alitaja.
Aidha Foya aliwashukuru wadau wa mashirika na kampuni mbali mbali wakiwemo Sanlam Insurance, GSM Group ambao ni wafadhili wakuu wa mbio hizo huku akiwataja wadau wengine kuwa ni pamoja na kampuni ya Vodacom Tanzania, Jubilee Allianz Insurance, Strategis Insurance na GardaWorld.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa huduma za Kinga kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dkt Crispin Kahesa alisema kupitia mchango wa mbio katika kipindi cha miaka mitano, taasisi hiyo imeweza kuwafikia wanawake takribani 200,000 kwenye wilaya 78 nchini sambamba na kuwajengea uwezo watoa huduma zaidi ya 250 ambao wanaendelea na uchunguzi pamoja na kuwahudumia wagonjwa wenye changamoto hiyo.
“Kila mwaka tunabaini wastani wa wagonjwa wapya 42,000 wa saratani kitaifa ambapo kati yao wagonjwa 14,000 ni wanawake wenye saratani ya mlango wa kizazi. Kati ya hao zaidi ya asilimi 90 wanafika wakiwa kwenye hatua ya tatu na ya nne ya ugonjwa hivyo tunapata matokeo ambayo sio mazuri kwenye tiba. ‘’
“Tunashukuru mbio hizi zimesaidia kuhamisisha jamii ijitokeze kufanya uchunguzi wa awali hasa wale wa vijijini. Tunaamini mchango utakaopatikana kwenye msimuu huu wa mbio utatusaidia kuwafikia kina mama zaidi ya 20,000,’’ alisema.
Wakizungumza kwa niaba ya wadhamini wengine wa mbio hizo, Kyenekiki Kyando kutoka Sanlam Insurance na Bi Rukia Yazid kutoka kampuni ya GSM Group walisema ushiriki wa taasisi hizo kwenye mbio hizo unatokana na kuguswa kwao na agenda pamoja na nia thabiti ya waandaaji wa mbio hizo katika kuokoa maisha ya wanawake na watoto nchini kupitia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi pamoja na afya salama ya wakina mama wakati wa kujifungua.
Usajili wa mbio za NBC Dodoma Marathon umefunguliwa rasmi hatua inayotoa fursa kwa washiriki kuweza kujisajili kupitia tovuti ya www.events.nbc.co.tz na kuchangia kiasi cha TZS 45,000 kwa usajili wa mtu mmoja mmoja au 42,000 kwa usajili wa kikundi chenye idadi ya watu 30 au zaidi.
ZINAZOFANANA
Meridianbet yazindua GATES OF OLIMPIA sloti ya kisayansi yenye ushindi wa kihistoria
MERIDIANBET yagusa mioyo ya watu, yafika Makumbusho, M’nyamala kutoa msaada familia zenye mahitaji
Njia 100 za ushindi na Fruit Salad 100 kasino