
THABO Mbeki Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini amewasili nchini Tanzania Mei 20, 2025, kushiriki Mhadhara wa Siku ya Afrika (Africa Day Lecture) ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania, ambao utafanyika jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Thabo Mbeki amepokelewa na Cosato David Chumi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mhadhara huo ambao ni wa 15 kuandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki, unatarajiwa kujadili kuhusu mustakabali wa Bara la Afrika na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wanataaluma, wadau kutoka Serikalini, viongozi wastaafu, vijana, na wawakilishi wa sekta binafsi.
Sambamba na Mhadhara huo, Rais Mstaafu Mbeki anatarajiwa kushiriki katika mijadala mbalimbali ikiwemo; mjadala kuhusu Uchumi wa Buluu na Utalii, mjadala wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu, halikadhalika majadiliano kuhusu Fursa ya Urais wa Afrika ya Kusini wa kundi la Nchi zenye Uchumi Mkubwa Duniani (G20) kwa ustawi na maendeleo ya Afrika.
Mhadhara wa Siku ya Afrika unafanyika nchini baada ya Taasisi ya Thabo Mbeki kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
ZINAZOFANANA
CBE yajivunia mchango wa wahitimu wake
MERIDIANBET yagusa mioyo ya watu, yafika Makumbusho, M’nyamala kutoa msaada familia zenye mahitaji
Brigedia Mwakamyanda kuzikwa kesho Mbeya