May 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

CBE yajivunia mchango wa wahitimu wake

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Profesa Edda Lwoga (katikati)

 

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kinatarajia kujenga maabara za kisasa zitakazoidhinishwa na mashirika ya kimataifa ya viwango ambazo zitakuwa kitovu cha mafunzo, utafiti, na ushauri wa vipimo katika Afrika Mashariki na Kati. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya vipimo duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka.

Alisema anaamini kwamba maabara hizo zitachangia maendeleo ya teknolojia na viwanda nchini huku akusema kuwa ndoto ya CBE ni kuendelea kukua na kuenea zaidi Tanzania na kimataifa.

“ Miongoni mwa malengo yetu kwa sasa ni kuanzisha programu mpya za kitaaluma zinazoendana na mahitaji ya sasa kwenye sekta ya vipimo na usanifishaji wa viwango (metrology), ikiwa ni pamoja na kuanzisha shahada ya Kwanza ya elimu ya Vipimo na Usimamizi wa Ubora (Bachelor in Metrology and Quality Management) ikifundishwa kwa njia ya uanagenzi (apprenticeship mode of delivery),” alisema

Alisema wanatarajia kuanzisha shahada ya Kwanza ya Uhandisi wa Vipimo Viwandani (Bachelor in Industrial Metrology Engineering) na kwamba kozi hizo zinazotarajiwa kujibu mabadiliko ya viwanda na teknolojia yanayohusisha uzalishaji bidhaa kisasa, udhibiti endelevu wa ubora na ubunifu.

“Kwa sasahivi tuna ushrikiano mzuri na tasisi mbalimbali zinazofanya kazi zinazohusisha vipimo mfamo TBS, Weights and Measures Agency (WMA) n,k. Lakini Ili kuimarisha mafunzo yetu ya vitendo, tunatazamia kuongeza ushirikiano na sekta ya viwanda, hasa katika viwanda vya uzalishaji, utengenezaji, na karakana za mitambo,” alisema.

Alisema ushirikiano huo utawapa wanafunzi wa chuo hicho uzoefu wa vitendo unaohitajika ili wawe wataalamu bora wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira la kisasa.

Profesa Lwoga alisema CBE inajivunia mafanikio ya wahitimu wake ambao kwa sasa wanafanya kazi kote nchini katika taasisi muhimu kama vile Tanzania Bureau of Standards (TBS), Weights and Measures Agency (WMA), Tanzania Railways Corporation (TRC), Tanzania Ports Authority (TPA) na Tanzania National Roads Agency (TANROADS) na Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC)

“Pia wahitimu wanatoa mchango wao katika maabara binafsi, kampuni za mafuta na nishati, na viwandani, kwa kuhakikisha ufanisi, usalama, na ubora kupitia vipimo sahihi,” alisema.

Profesa Lwoga alisema siku ya vipimo duniani ni fursa ya kuangazia umuhimu wa vipimo sahihi kama msingi wa usawa, maendeleo ya kiuchumi, na ustawi endelevu na kwamba CBE itaendelea kutoa wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu ili kuunga mkono maendeleo ya Tanzania na duniani.

About The Author

error: Content is protected !!