May 19, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Madaktari Bingwa wa Samia toeni huduma nzuri kwa wananchi

ZUWENA Omary, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi ametoa wito kwa madaktari bingwa wa Rais Samia kutoa huduma bora na tarajiwa kwa ufanisi mkubwa na kutoa muongozo sahihi kwa wagonjwa wanaohitaji huduma ili kuhakikisha kila mwananchi anafurahia uwepo wa kambi ya huduma za kibingwa. Anaripoti Joyce Ndeki, Lindi … (endelea).

RAS Zuwena ameyasema hayo leo, Mei 19, 2025 mkoani Lindi wakati akiwapokea na kufungua rasmi kambi ya madaktari bingwa wa Rais Samia katika hospitali za halmashauri zote sita(6) za mkoa huo.

Amesema wananchi wanaokwenda kuhudumiwa na madaktari hao ni wa kawaida kutoka kwenye mazingira yao, hivyo ni matarajio yake kuwa madaktari bingwa watakuwa wavumilivu wakati wote wa kutoa huduma ili kufikia kila atakayefika kituoni kupata huduma.

“Niwashukuru na kuwapongeza madaktari bingwa kwa kuwa timu teule ya Samia  kwa ajili ya kutekeleza dhamira ya Rais ya kila Mtanzania kupata huduma bora za afya za kibingwa kwenye maeneo yao, sisi wananchi huku bila uwepo wenu wataalam wa afya hakuna maisha, tunaomba mtuvumilie na kutuhudumia kwa upendo,” amesema Zuwena

Zuwena ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Lindi wenye changamoto za kiafya kutumia fursa hiyo ili kupata huduma za kibingwa na kwa wananchi ambao sio wagonjwa kwenda kufanya uchunguzi wa afya zao, huku akiwaonya kutosubiri muda kuisha.

“Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania amejenga vituo vingi vya afya, miundombinu, vifaa tiba na kuhakikisha watumishi wa sekta ya afya wengi wanaajiriwa kwa kutambua umuhimu wa kusogeza huduma za kibingwa na bobezi ndio maana ameamua kuendelea na zoezi hili la madaktari bingwa ili Watanzania wote wapate huduma za afya karibu na maeneo yao na kuwapunguzia gharama,” amebainisha Zuwena

Akitoa salamu za Wizara ya Afya, Michael Mbele, Afisa program kutoka Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto amesema kambi ya madaktari bingwa 47  itakuwa katika hospitali za halmashauri zote za mkoa wa Lindi, lengo likiwa ni kuwafikia wananchi wenye uhitaji na huduma za kibingwa sambamba na kutoa mafunzo kazini kwa wahudumu wa afya katika maeneo yao ya kazi.

About The Author

error: Content is protected !!