May 16, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yazindua kampeni ya “NBC Shambani’’ kwa wakulima wa Ufuta Lindi, Mtwara

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC), imetambulisha kampeni yake ya ‘Wekeza NBC Shambani Ushinde’ kwa wakulima wa zao la ufuta mkoa wa Lindi na Wilaya za Masasi na Nanyumbu mkoani Mtwara huku ikikisistiza dhamira yake ya kuunga mkono azma ya serikali ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka asilimia 5 hadi 10 ifikapo mwaka 2030. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mtwara … (endelea).

Hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo imefanyika leo mkoani Lindi ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva. Pia walikuwepo wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara akiwemo Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Lindi Keneth Shemdoe, viongozi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika vya wakulima na wafugaji (AMCOS), pamoja na wadau wengine wanaoshiriki kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo.

Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Biashara wa benki ya NBC, Joseph Lyuba na Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo na wakulima kutoka Benki ya NBC, Raymond Urassa waliwaongoza maofisa wengine wa benki hiyo kwenye uzinduzi wa kampeni ambayo ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kupitia uchumi jumuishi unaochagizwa na huduma rasmi za kifedha.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwanziva aliitambua benki ya NBC kama mdau muhimu kwenye maendeleo ya sekta ya kilimo nchini hususani mikoa ya kusini ambapo benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuendesha kampeni za namna hiyo zenye lengo la kuchochea kasi ya uzalishaji wa mazao ya korosho na ufuta sambamba na kuwajengea uelewa wananchi kuhusu elimu ya fedha.

“Nimefarijika sana kuona kwamba kupitia kampeni hii NBC zaidi ya milioni 30 zimetengwa kwa ajili ya zawadi mbalimbali mahususi kwa wakulima ikiwemo vitendea kazi vya shughuli za kilimo. Hamasa hii ni msaada mkubwa kwa serikali kwa kuwa kilimo kinaongeza ajira na zaidi elimu wanayoipata wakulima kupitia kampeni ni msaada zaidi katika kufanikisha azma ya kilimo cha kisasa sambamba na kuongeza uelewa wa masuala ya fedha kwa wananchi…tunawashukuru sana NBC,’’ alisema.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Lyuba alisema ili kufanikisha dhamira yake ya kuunga mkono azma ya serikali ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka asilimia 5 hadi 10 ifikapo mwaka 2030, benki hiyo inaendelea kubuni na kuboresha huduma mbalimbali za kifedha kwa ajili ya wadau mbalimbali wa sekta kilimo nchini wakiwemo wakulima.

“Kupitia kampeni kama hizi, pamoja na zawadi mbalimbali zinazolenga kuwavutia wakulima tunajitahidi zaidi kuwekekeza kwenye suala zima la elimu ya fedha kupitia maofisa wetu waliobobea kwenye masuala ya kilimo, bima za afya na kilimo, huduma za kidigitali katika kufanikisha miamala kwa wakulima pamoja na mikopo ya mitaji na zana za kilimo. Tunaamini kupitia kasi hii tuliyo nayo hadi kufikia 2030 hali ya ukuaji wa sekta ya kilimo nchini itakuwa ya kuridhisha zaidi,’’ alisema,

Akizungumzia kampeni hiyo ya miezi miwili, Urassa alisema inatoa fursa kwa wakulima wa zao la ufuta mkoa wa Lindi na Wilaya za Masasi na Nanyumbu mkoani Mtwara kushinda zawadi mbalimbali ikiwemo pikipiki na kompyuta mpakato ‘Laptops’, huku akitaja kuwa walengwa ni wakulima wa zao la ufuta kupitia vyama vya msingi, vyama vikuu vya ushirika na mkulima mmoja mmoja ambao wanahudumiwa na benki hiyo.

“Lengo la kampeni hii ni kuwahamasisha wakulima wa zao la ufuta kwenye mkoa wa Lindi na Mtwara kutunza fedha zao kwenye mifumo rasmi ya kifedha hasa benki badala ya kutunza kwenye mifumo isiyo rasmi. Tunawakaribisha sana kufungua akaunti zao za NBC Shambani ili wawe kwenye nafasi ya kushinda zawadi hizi zikiwemo pikipiki na ‘laptop,’’ alisema.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzao, Bakari Salumu na Hawa Rashidi waliwahimiza wakulima wenzao kutoka mikoa hiyo miwili kutumia vema ujio wa kampeni hiyo kujinufaisha kupitia fursa mbalimbali zinazoambatana na kampeni hiyo ikiwemo zawadi, elimu ya fedha, mikopo na huduma nyingine ikiwemo bima za afya na mazao.

About The Author

error: Content is protected !!