May 16, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yakabidhi Kombe la Ubingwa wa NBC Championship kwa Mtibwa Sugar

 

MDHAMINI Mkuu wa Ligi Daraja la Kwanza (NBC Championship) Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi kombe la ubingwa wa ligi hiyo kwa timu ya Mtibwa Sugar FC yenye maskani yake Turiani, Mkoani Morogoro ambayo ndiyo bingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa 2024/2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua hiyo inatoa ruhusa kwa mabingwa hao kushiriki Ligi Kuu ya NBC (NBC Premiere League) katika msimu ujao wa 2025/2026 sambamba na timu Mbeya City FC kutoka jijini Mbeya ambayo imemaliza ligi hiyo ikiwa nafasi ya pili.

Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa huo ilifanyika jana katika uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es Salaam ikipambwa na mechi ya hisani kati ya bingwa huyo na timu ya Mbeya City FC, mechi iliyoisha kwa timu hizo kutoka suluhu ya 2-2.

Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na Wakubwa wa benki ya NBC, Elibariki Masuke alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi kwenye tukio hilo lililopambwa na uwepo wa wadau mbalimbali wa mchezo huo wakiwemo viongozi wa kisiasa na serikali pamoja na viongozi mchezo huo wakiongozwa na Makamu wa pili wa Rais wa TFF na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Steven Mguto.

Akizungumza kwenye makabidhiano hayo, Mguto pamoja na kupongeza jitihada za benki ya NBC katika kukuza mchezo soka nchini kupitia udhamini wake wa ligi tatu muhimu ikiwemo Ligi Kuu ya NBC, NBC Championship na Ligi ya Vijana alionyesha kuvutiwa na ongezeko la ushindani baina ya vilabu vinavyoshiriki ligi hizi, ushindani aliosema unatokana na udhamini mzuri unaoviwezesha vilabu hiyo kujiendesha kwa ufasaha zaidi sambamba na kusajiri wachezaji bora zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.

“Ligi ya Championship imekuwa ni ligi bora si tu kwa kile wanachokionesha wachezaji uwanjani bali pia hata kiuendeshaji ni ligi ambayo haitusumbui sana. Ikumbukwe kwamba hapo awali changamoto zilikuwa ni nyingi ikiwemo ukata miongoni mwa timu shiriki kutokana na ukweli kwamba timu nyingi zinazoshiriki ligi hii zilikuwa zinategemea misaada ya wadau mitaani huko huko jambo ambalo kwasasa Benki ya NBC kama mdhamini wa ligi hii imeweza kusuluhisho na kuleta utulivu…tunawashukuru sana NBC na tunawapongeza sana Mtibwa Sugar na Mbeya City mafanikio haya,’’ alisema.

Kwa upande wake Masuke alisema benki hiyo inayodhamini ligi tatu muhimu hapa nchini kwa udhamini wenye thamani ya Sh. 32 bilioni itaendelea kuboresha zaidi ligi hizo ili ziendelee kutoa matokeo chanya kitaifa na kimataifa kulingana na malengo ya udhamini huo ikiwemo suala zima la kuzalisha ajira ambapo kwasasa zaidi ya ajira 7,000 za moja kwa moja zimezalishwa kupitia udhamini huo.

“Tunawapongeza sana washiriki wote wa ligi ya Championship lakini kiupekee zaidi tunawapongeza Mtibwa Sugar FC kwa kuibuka washindi kwenye ligi hii. Pongezi zetu pia tunazielekeza kwa Mbeya City FC kwa kuwa mshindi wa pili na hivyo nae pia anakwenda kushiriki Ligi kuu ya NBC msimu ujao…hongereni sana,’’ alisema Masuke .

Kwa mujibu wa Masuke benki hiyo inajivunia sana mafanikio ya vilabu vinavyofanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa huku akibainisha kuwa mafanikio hayo yanatokana na ushindani bora uliopo kwenye ligi za ndani.

“Kwetu mafanikio hayo ni kama motisha ya kuedeleza zaidi jitihada za kuioboresha zaidi ligi hizi zote tatu kupitia udhamini na utoaji wa huduma za kifedha mahususi kwa wadau wake ikiwemo mikopo ya vyombo vya usafiri kwa vilabu, bima za afya kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi pamoja utoaji wwa elimu ya fedha kwa wachezaji na vilabu shiriki.

Akizungumzia ubingwa huo Nahodha wa Mtibwa Sugar FC, Oscar Masai pamoja na kuwashukuru wadau wote kwa jitihada zao zilizosaidia kufanikisha ubingwa huo akiwemo mdhamini huyo kwa kuandaa mazingira mazuri kwa timu zote shiriki, aliahidi kwa niaba ya wachezaji wenzake kuhakikisha wanajipanga vema ili waweze kutoa ushindani zaidi kwenye ligi kuu ya NBC msimu ujao.

About The Author

error: Content is protected !!