May 8, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Chatanda ashuhudia utiaji saini wa Bil 13.3 kuboresha miundombinu Rufiji

MWENYEKITI wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mitano ya Sh. 13.3 bilioni zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja wilayani Rufiji. Anaripoti Joyce Ndeki, Pwani … (endelea). 

Tukio hili la utiaji saini limefanyika Mei 7, 2025 mara baada ya kukamilika kwa ziara ya siku mbili ya Chatanda kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo, katika eneo la uwanja wa stendi wa Ikwiriri  na kushuhudiwa  na maelfu ya wananchi wa wilaya  hiyo huku wasanii kadhaa wakitumbuiza kwa burudani za muziki.

Akitoa taarifa ya miradi hiyo, Meneja wa Wakala za Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Pwani, Leopold Runji amefafanua kuwa gharama hizo zinahusisha ukarabati wa barabara ya Nyamwage yenye Kilomita 28, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Chumbi- Kiegele yenye kilomita 1.4, ukarabati wa barabara ya Mohoro- Mtanga kilomita 12.3 na Mohoro Ndundutawa yenye kilomita 7.5.

Pia ukarabati wa barabara ya Nyamwage- Mpakani- Nambunju na ujenzi wa  barabara za lami katikati ya mji wa Ikwiriri ambapo amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia  kuiunganisha  wilaya  hiyo na maeneo mbalimbali ya mikoa ya Tanzania.

Chatanda amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za miradi na kufafanua kwamba  kwa kufanya hivyo siyo tu ametekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa mafanikio  makubwa  bali ameleta  mapinduzi katika  sekta  ya miundombinu kote nchini.

Amempongeza Mchengerwa kwa kusimamia utekelezaji wa miradi  yote kwa kiwango cha juu huku akitoa wito  kwa maeneo  mengine nchini kuiga utekelezaji huo.

”Ndugu zangu hapa ni vema tuwe wakweli, unaweza ukaletewa  fedha  za maendeleo  lakini ukashindwa kutekeleza lakini,hivyo nampongeza  mbunge wenu kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hii ambayo inakwenda kuleta tija kubwa kwa wananchi  katika Wilaya ya Rufiji,” amefafanua Chatanda

Mbali na  kukagua  miradi  ya Serikali pia ameshuhudia ujenzi wa  nyumba ya mtumishi  wa chama, pia ameshuhudia mradi mkubwa wa ujenzi wa ukumbi wa kisasa  wa wilaya unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.5 unaofadhiliwa na Mbunge wa Rufiji Mhe. Mchengerwa kwa kupitia marafiki na wadau mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu miradi ya elimu katika wilaya hiyo, Chatanda amesema amefurahishwa na kazi nzuri ya ongezeko kubwa la Shule za Msingi na Sekondari na kutoa wito kwa wananchi kuwapeleka watoto wao  katika shule  hizo ili kuunga mkono  maono ya Mhe. Rais ya kuwakomboa wananchi kielimu pia kwa manufaa makubwa ya taifa na vizazi vyao.

Mbunge wa Rufiji Mchengerwa  amesisitiza kuwa Serikali imefanya  kazi kubwa ya ujenzi wa shule ambapo amesema  wakati anaingia kwenye ubunge kulikuwa na  na Shule za Msingi 40 tu ambapo sasa kuna shule 63 na upande wa Vituo vya Afya, awali  kulikuwa na vituo 3 na sasa  vimefika 9, huku asimshukuru Mhe. Rais Samia kwa maono makubwa  ya kuwaletea  maendeleo watanzania.

Aidha, Chatanda alipotembelea  na  kukagua  ukarabati wa hospitali ya Wilaya  ya Rufiji na ujenzi wa kichomea taka  katika eneo la Utete  uliogharimu takribani Sh. 900 milioni na kuwataka  wananchi kutumia  huduma hizo ikiwa ni pamoja na wanaume kuwa msitari wa mbele kuwapeleka wake zao  kwenye  huduma za kliniki ili kujua afya za wenza wao na watoto.

Akizungungumzia kuhusu ukatili wa kijinsia, amewataka wazazi  kuwalea watoto wao katika misingi maadili  ili waweze kuja  kuwa wazazi bora badala ya kuwaacha  kujifunza kwenye  mitandao.

About The Author

error: Content is protected !!