
DK. Rashid Mfaume, Mkurugenzi wa Idara ya Afya Lishe na Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema kutokana na uhaba wa maeneo katika Jiji la Dar es Salaam ni vyema Halmashauri zifikirie kujenga majengo ya kutolea huduma za afya kwa muundo wa gorofa. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).
Dk. Mfaume amesema hayo wakati alipotembelea kituo cha afya cha Kinondoni kwenye ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii katika Manispaa ya Kinondoni, Mkoani Dar es salaam.
“Kutokana na uhaba wa maeneo kwenye Mkoa wetu ni vyema sasa tukafikiria kujenga vituo vya kutolea huduma za afya kwa muundo wa gorofa hata kama tutajenga kwa awamu,” amesisitiza.
Aidha, Dk. Mfaume amevielekeza vituo vya afya vyenye mapato makubwa yatokanayo na wananchi kuchangia huduma kutumia mapato hayo katika kutekeleza miradi mbalimbali ili kufanikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi ikiwemo ununuzi wa vifaa tiba.
“Niwapongeze kituo cha afya cha Bunju kwa kutumia fedha za mapato ya ndani zaidi ya Sh. 172 milioni kununua vifaa tiba, na nivielekeze vituo vyenye mapato makubwa pia kuiga mfano huu wa kituo cha afya cha Bunju” amesisitiza.
Ameongeza kuwa, katika kuelekea utekelezaji wa huduma ya Bima ya Afya kwa wote ni lazima vituo vyote vya afya kuwa tayari kwa ajili ya kuwahudumia wanachama hao kwa huduma mbalimbali.
ZINAZOFANANA
Waziri Mkuu Majaliwa aonyesha maendeleo katika huduma ya Afya
Serikali yawakumbuka wagonjwa figo
Wizara ya Afya kuchunguza sakata la mama kubadilishiwa mtoto