May 1, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Tanzania yakanusha ukiukwaji wa Sheria kesi ya Tundu Lissu

Tundu Lissu, Mwenyekiti Chadema

 

SERIKALI ya Tanzania imesema hakuna sheria iliyokiukwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam ilipoamua kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu kwa njia ya mtandao. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2025/26. “Ukifuatilia kilichotokea tarehe 24, Procedures (taratibu) zile zilikuwa properly lollowed (zimefuatwa inavyotakiwa), sasa huyu mtu anayetokea anayesema kuna uvunjifu wa sheria, sheria ipi sheria si ndiyo hii?,” alihoji Johari na kuongeza: “hii ndiyo sheria, na mimi ninayezungumza hapa ndiye Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”

Akifafanua zaidi, Johari alisema Mahakama inaweza kuendesha kesi kwa njia ya mtandao iwapo imeona kuna tishio lolote baada ya kufanya tathmini.

“Mahakama itaassess (tathmini) mazingira yaliyopo siku hiyo na kuona kwamba tuisikilizeje shauri hili na hasa kama kuna mazingira katika mitandao zinarushwa habari za ajabu ajabu zingine ni za kutisha, kwa hiyo mahakama iki-assess (tathmini) mazingira inaweza kuamua, na ni kwa mujibu wa sheria,” alieleza.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, alizungumzia suala hili kwa kusema kuwa huduma ya Mahakama Mtandao itaendelea, hasa kunapokuwepo na viashiria vya matishio ya kiusalama.

“Kama kuna matishio, kwa mfano wenzetu walikuwa wanasema kwenye maandamano wanaenda kukinukisha na kwa sababu za kiusalama ikaonekana ni vizuri kesi ikasikilizwa kwa njia ya mahakama mtandao,” alisema Bashungwa jijini Dodoma, alipoambatana na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), kukagua Makasha ya kisasa ya Mahakama Mtandao yanayowezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya kiteknolojia katika Gereza la Isanga, Dodoma.

Hata hivyo Maelezo haya ya Serikali yamekosolewa na baadhi ya watu, ikionekana kama kuingilia Muhimili wa Mahakama ambao umepanga kutoa maamuzi Mei 6, 2025. Mmoja wa waliokosoa kupitia mtandao wake wa X ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche.

“Nilifikiri uamuzi wa kutumia mtandao kwenye kesi ya Lissu ni uamuzi wa Mahakama. Anachozungumza Bashungwa ni kama maamuzi hayo walifanya wao. Anasema hatuwezi kuruhusu!!! Bashungwa ni nani kwenye kesi hii?”, alihoji Heche.

Aprili 24, 2025, Lissu ambaye pia ni mwanasheria alipinga kesi yake kusikilizwa siku hiyo kwa njia ya mtandao akitaka iwe ya wazi, huku wanasheria wake wakiongozwa na Peter Kibatala wakisema utaratibu uliotumika kutaka kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya mtandao umekiuka sheria.

Kufuatia mabishano ya kisheria mahakamani hapo kati ya upande wa utetezi na ule wa mashitaka wakiwemo mawakili wa serikali, Mahakama ilisema itatoa uamuzi Mei 6, iwapo kesi hiyo itaendeshwa kwa njia ya mtandao ama mshitakiwa huyo ataletwa Mahakamani.

Kabla ya kuahirishwa kwa kesi, nje ya Mahakama kulitokea mzozo kati ya Polisi na viongozi na wafuasi wa CHADEMA waliopanga kwenda kusikiliza kesi hiyo, ambapo CHADEMA kupitia kwa Katibu Mkuu wake, John Mnyika, ilidai kukamatwa kwao na karibu watu 24 walipatwa na majeraha.

Polisi ilikiri kuwakamata baadhi ya viongozi akiwemo Makamu Mwenyekiti, John Heche na Katibu Mkuu, Mnyika.

Kwa mara ya kwanza Lissu alifikishwa Mahakamani Aprili 10, na kusomewa mashtaka ya uchapishaji wa taarifa za uongo na uhaini katika Mahakama ya Kisutu.

About The Author

error: Content is protected !!