
Othman Masoud Othman
WAKATI Tanzania ikiadhimisha miaka 61 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman amesema ipo haja ya kufanyika kwa mabadikiko mkubwa ya mfumo wa Muungano ili Nchi zote mbili za washirika zipate haki sawa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pemba … (endelea).
Othman ameyasema hayo leo tarehe 26 Aprili 2025, katika ukumbi wa Samael Chakechake, Pemba alipokuwa akizungumza na maelfu ya vijana wa chama hicho katika kongamano maalumu la maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano.
Alisema uwepo wa Muungano huu kwa muda mrefu unaikandamiza Zanzibar licha ya kuwa na rasilimali zake nyingi inashindwa kupata maendeleo na kukuza uchumi kama nchi huru.
Alisema pamoja na uwepo wa kasoro nyingi za Muungano na kulalamikiwa, watawala wanashindwa kujali na wamekuwa wakiongeza mambo mengine mapya kujinufaisha na familia zao.
“Tulianza kulalamimia mambo 11 ya Muungano hapo awali lakini sasa tunalalamikia mambo 41 bila wenzetu kujali lolote huku mambo yote hayo yakinufaisha upande wa pili wa Tanzania Bara,” alisema.
Aidha Othman ambae pia ni Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar amesema kwa nyakati tofauti viongozi mbalimbali wamekuwa wakifanya jitidaha kumaliza, changamoto hizo lakini hakuna mafanikio ambayo yanapatikana kwa sababu wenye nguvu ndio wenye maslahi.
“Zimeundwa zaidi ya kamati 10 kushughulikia kero za Muungano lakini zote zimeishia njiani na hakuna kilichotimia hadi leo na ndio maana tunasema wenzetu hawana ukweli,” alisema.
Sambamba na hilo alisisitiza changamoto hizo zinaiathiri zaidi Zanzibar ikiwemo kukosa mamlaka ya kukopa nje ya nchi fedha ambazo zingeweza kuendesha miradi na kukuza uchumi wa Zanzibar.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa shama hicho, Ismail Jussa amesema Muungano wa Zanzibar na Tanganyika umekuwa na vikwazo vingi, kwa muda mrefu ambavyo viongozi mbalimbali wamevisemea.
Alisema vikwazo hivyo ni pamoja na kukosekana kwa usawa na nchi zote mbili washiriki ambazo kabla kuundwa kwa Muungano huo zilikua nchi huru.
“Nyinyi vijana wakati tunaadhimisha miaka 61 hii ya Muungano ni lazima mfahamue vita hii haikuanza leo na nyinyi muna wajibu wa kuendeleza mpaka tutakapoleta heshima ya Zanzibar kuwa nchi huru yenye haki na usawa katika Muungano huu.
Sambamba na hayo Jussa alisema watawala waliilazimisha Zanzibar kuingia kwenye Muungano bila ya wahusika kurusika.
Akitoa salamu za vijana Makamu Mwenyekiti Ngome ya vijana Taifa wa chama hicho, Nassor Ahmed Marhoun alisema vijana wapo tayari kuendelea kupambana kwa njia za kidemokrasia.
Alisema njia pekee ya kuzifanya Zanzibar kupinga hatua zaidi za kimaendeleo ni lazima washirikiane kwa pamoja kuiondoa CCM madarakati katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.
ZINAZOFANANA
Shirika la Amnesty kuchunguza matukio ya wafuasi wa Chadema kupigwa Kisutu
Mahakama: Kesi ya Lissu kuendelea kusikilizwa kwa njia ya mtandao
Tundu Lissu agoma kusikiliza kesi yake kwa njia ya mtandao