
SHIRIKA la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, limekutana na kufanya mahojiano na baadhi ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambao walijeruhiwa mara baada ya kukamatwa mahakamani Kisutu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)
Wanachama pamoja na viongozi hao walikamatwa mara baada ya kujitokeza mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi zinazomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, ambayo siku ya jana tarehe 24 Aprili 2025, iliitwa kwa ajili ya kutajwa.
Wawakilishiwa Shirika hilo walifika kwenye makao makuu ya chama hicho mapema hii leo na kukutana na kufanya mazungumzo na makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, John Heche na Naibu Katibu Mkuu- Bara, Amani Golugwa.
Baada ya mazungumzo hayo Amnesty wakiwa na mwenyeji wao Wakili Jebra Kambole, walipata nafasi ya kukutana na wanachama waliokutana na kadhia hiyo kwa kuwaelezea nini kilichojiri.
Roland Ebole mmoja wa wawakilishi hao, aliwaambia waandishi wa Habari kuwa matukio hayo yanaonesha kulikuwa na uvunjifu mkubwa wa Haki za Binadamu na kusema kuwa shirika hilo linaanzisha uchunguzi rasmi dhidi ya Jeshi la Polisi la Tanzania ili kuona ni kwa namna gani limekuwa likikiuka Haki za Binadamu kwa kuwatesa raia wasiokuwa na hatia.
Aliendelea mbele kwa kusema kuwa, shirika hilo limesikitishwa na kulaani vikali na tuhuma hizo zinazoelekezwa kwa Jeshi la Polisi kwani kiuhalisia Polisi wanapaswa kutumika kuwa wapatanishi, na wachunguzi badala ya kufanya matendo kama hayo yanayoingia moja kwa moja kwenye uvunjifu wa Haki za Binadamu na kuondoa dhana ya utawala bora kwa Taifa.
“Mahakama zinafaa kuwa huru, ziwaruhusu wananchi wanaotaka kuhudhuria kesi, mambo tuliyoshuhudia jana vyombo vya dola waliwadhulumu wale waliokuja mahakamani kuhudhuria kesi ya Tundu Lissu.”
“Kuna ripoti tumepokea kuwa kuna watu walichapwa na kujeruhiwa, pia tutachunguza kisa ambacho kimeropitiwa kuwa mmoja ya waliofika mahakamani alipigwa na kupelekea kufariki, mambo haya tukiyathibitisha tunaweza kusema kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,” alisema Ebole
Alipoulizwa endapo ziara yao hapa nchini italenga kukutana na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama au viongozi wa serikali kwa ujumla wake, Ebole amesema kwa sasa hawafikirii kufanya hivyo kwani wanatarajia kukutana na viongozi hao pindi uchunguzi wao utakapokamilika na ripoti ya uchunguzi kutoka.
Katika ziara hiyo Ebole, ameambatana na Wakili kutoka Uganda Andrew Karamang, Godwin Toko kutoka Shirika la AGORA Uganda na Mjumbe wa Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria Kenya (KLS) Wakili Gloria Kimani.
ZINAZOFANANA
Mahakama: Kesi ya Lissu kuendelea kusikilizwa kwa njia ya mtandao
Marekani kumkamata Traoré?
Tundu Lissu agoma kusikiliza kesi yake kwa njia ya mtandao