April 23, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Exim yakabidhi madarasa kwa shule mbili za Sekondari Kigoma

KATIKA juhudi za kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu nchini Tanzania, Benki ya Exim Tanzania imekabidhi rasmi madarasa kwa shule mbili za sekondari wilayani Buhigwe katika mkoa wa Kigoma. Shule hizo, shule ya Sekondari Kaphunya na Shule ya Sekondari Nyakitundu, zimepokea madarasa hayo yaliyokamilika yenye viti na madawati, ikiwa ni sehemu ya juhudi endelevu za benki hiyo katika kusaidia sekta ya elimu na kuboresha matokeo ya kujifunza kote nchini. Pia benki hiyo imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya michezo kwa shule hizo mbili kama sehemu ya kuchangia maendeleo ya sekta ya michezo nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Stanley Kafu, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, alisisitiza dhamira ya benki hiyo katika kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini.

“Sisi kama Benki ya Exim, tunaamini kuwa elimu ni msingi wa maendeleo katika jamii yoyote ikiwemo Tanzania. Kwa kuwekeza katika mazingira ya kujifunzia, hatujengi tu madarasa na kutoa madawati haya, bali tunaunda mustakabali wa vijana wetu na kuwawezesha jamii. Tunajivunia pia kuchangia maendeleo ya sekta ya michezo kwa vijana wetu kwa kutoa vifaa vya michezo maana ni sehemu ya kuimarisha afya zao ili waweze kusoma vizuri,” alisema Kafu.

Mbali na sekta ya elimu, benki ya Exim imekuwa ikishiriki kikamilifu katika miradi mbalimbali ya uwajibikaji kwa jamii kupitia mpango wake unaojulikana kama ‘Exim Cares’. Benki hiyo imechangia kuboresha huduma za afya kwa kutoa vifaa tiba kwa hospitali na vituo vya afya mbalimbali nchini, imewezesha ujumuishaji wa kifedha kupitia suluhisho za benki za kidijitali, na pia kushiriki katika jitihada za utunzaji wa mazingira.

Naye Mkuu wa wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, kwa niaba ya Mgeni Rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, aliipongeza Benki ya Exim kwa mchango wake mkubwa katika kusaidia juhudi za serikali za kuboresha upatikanaji wa elimu bora.

“Mchango huu wa madarasa, vitu na madawati yake kutoka Benki ya Exim ni uthibitisho wa nguvu ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kuendeleza na kufikia malengo ya taifa. Madarasa haya yatatoa mazingira bora ya kujifunza kwa watoto wetu, kuwawezesha kufaulu kitaaluma na kujenga maisha yao ya baadaye. Tunatoa wito kwa wadau wengine kuungana nasi katika kuinua sekta ya elimu,” alisema Mhe. Ngayalina.

Sekta ya elimu nchini inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uchache wa walimu, ukosefu wa maabara, na upungufu wa madarasa katika shule mbalimbali zikiwemo shule ya Sekondari Kaphunya na Shule ya Sekondari Nyakitundu. Mazingira haya yanaathiri ubora wa elimu na kupunguza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na hivyo kuathiri kiwango cha elimu nchini.

Madarasa haya mapya yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuboresha mazingira ya kujifunza kwa wanafunzi wa sekondari katika mkoa wa Kigoma. Benki ya Exim inaendelea kujitolea kuleta mabadiliko chanya kwa kushirikiana kwa karibu na serikali za mitaa na serikali kuu ili kuchochea maendeleo.

“Kwa madarasa haya, hatujengi tu majengo, bali tunajenga mustakabali ambapo kila mwanafunzi anapata fursa ya kujifunza, kukua, na kutimiza ndoto zake. Benki ya Exim itaendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa jamii kupitia elimu na sekta nyinginezo—kwa sababu tunapowekeza katika elimu, tunawekeza katika mustakabali wa Tanzania,” aliongeza Stanley.

Wakati huo huo, benki hiyo pia ilikabidhi vifaa mbalimbali vya michezo kwa shule zote mbili ikiwa ni moja maeneo ambayo yanakabiliwa na chagamoto ikiwemo upungufu wa vifaa vya michezo, wataalamu na viwanja vya michezo katika shule nyingi za msingi na sekondari nchini.

About The Author

error: Content is protected !!