April 22, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Shamba la Pinda labadili mtazamo wa wanafunzi Aniny Nndumi

 

UKIMUULIZA mwanafunzi  wa shule yoyote ya msingi kwamba ndoto yake anataka kuwa nani, atakutajia vyeo na kazi  anazoamini kuwa nzuri, lakini hata kuambia anataka kuwa mkulima. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mtazamo hasa kuhusu kilimo, ndio umesababisha hadi leo sekta hiyo kuonekana ya watu wa chini, wanaoishi vijijini na haiwezi kumpa mtu mafanikio,jambo ambalo sio sahihi kwani kuna wakulima, wakiwemo vijana waliojiajiri na kupata utajiri kupitia kilimo.

Lakini ziara ya kitaaluma ya wanafunzi wa shule ya msingi ya Aniny Nndumi ya Kimara jijini Dar es Salaam, iliyofanyika hivi karibuni mkoani Dodoma imebadili mtazamo wa wanafunzi hao kuhusu kilimo.

Wanafunzi wa shule hiyo ya msingi maarufu inayoongozwa na Mwalimu Mkuu, Erasto Joseph, hivi karibuni walifanya ziara ya siku tano mkoani Dodoma.

Katika ziara hiyo ya aina yake,  walitembelea shamba la Waziri Mkuu Mstaafu, Pinda (Pinda Farm), walitembelea Bunge na kushuhudia shughuli mbalimbali za Bunge, walifika kituo cha Watoto Yatima cha Bigwa mkoani Morogoro, walitembelea hifadhi ya Mikumi na kujifunza mambo mengi ambayo bila shaka yamewafungua macho na akili zao.

Mwanafunzi Reginald Martin alisema kuwa anatamani kumiliki shamba kubwa kama la Waziri Mkuu Mstaafu Pinda.

Anasema anapenda kumiliki shamba kama la Mzee Pinda kwa sababu, kwanza ni shamba kubwa, pili lina mambo mengi na kwamba anaamini akimiliki mifungo mingi ya ng’ombe, mbuzi, samaki, sungura na wengine, anaweza kuwa tajiri mkubwa  nchini kama alivyokuwa Mzee Reginald Mengi.

“Shamba la Pinda, kwanza ni kubwa sana, tumetembea hadi tumechoka, kuna mifugo mingi, ng’ombe, mbuzi, samaki, sungura, kuku. Kuna samaki wengi na wakubwa sana, yaani ukiangalia hadi raha,” anasema mwanafunzi huyo wa darasa la nne.

Mwanafunzi mwingine Elisha Baraka, anasema hajawahi kuona shamba kubwa zuri kama la Mzee Pinda na siku moja akiwa mkubwa, anatamani kumiliki shamba kama hilo.

“Shambani kwa Pinda nimeenjoy sana, tumeingia bungeni, tumetembelea maeneo mengi, lakini ziara ya shambani kwa Pinda, nimeipenda zaidi. Tumepata maelezo mazuri kuhusu shamba hilo na nimeandika kila kitu tulichoambiwa na kiongozi wa shamba hilo, nikiwa mkubwa nitakuwa na shamba kama la Pinda,” anasema Baraka.

Wanafunzi Dyaline Maiba na Athuman Mawazo, wote wa darasa la saba, kila mmoja kwa nyakati tofauti wanasema wanataka kuwa wanasiasa baada ya kutembelea Bunge.

“Nimefurahi kuingia bungeni, nimefurahi kumewona Waziri Mkuu na mimi siku moja nataka kuwa mwanasiasa, nataka kuwa Waziri Mkuu kama Kassim Majaliwa, anasema Dyaline.

Akitoa maelezo, kiongozi mkuu wa Pinda Farm, aliyejitambulisha kwa jina moja la Peter, anasema uwepo shamba hilo, unavutia watu wengi wanaofika mjini Dodoma kuja kwenye shamba hili.

“Hili shamba limekuwa kama sehemu ya utalii, tunapata wageni wengi kila siku ambao wanakuja kujifunza na baadhi wameanzisha mashamba yao,” anasema Peter.

Akizungumzia shamba la Samaki, Peter anasema bwala hilo lina uwezo wa kuhifadhi zaidi ya samaki 30,000  na samaki wa chini anavuliwa akiwa na uzito wa kilo moja na kuuzwa kwa sh 10,000.

“Tuna mabwawa mengi na tunazidi kuanzisha wengine, lengo letu ni kwamba shamba hili liweze kutoa samaki kila siku wa kuweza kulisha mji mzima wa Dodoma na hilo linawezekana,” anasema Peter.

Peter anasema moja ya faida ya shamba hili ni kwamba limetoa ajira ambapo vijana wengi wanaozunguka eneo hili, wamepata ajira za kudumu na wengine za muda.

Akizungumzia ziara hiyo, Mwalimu Mkuu  Erasto Joseph amesema lengo la ziara yao na kutoa fursa kwa wanafunzi kujifunza mambo mengine nje ya shule.

“Kwa mfano wamekuja bungeni, wameona shughuli za Bunge zinavyoendeshwa na kuanzia hapo kuna baadhi yao wanatamani kuwa Wabunge, Mawaziri au Spika na bila ndoto zao zinaweza kuanzia hapa Bungeni.

“Tumefika shambani kwa Pinda, wengine wamesema wanatamani kuwa wakulima kama Mzee Pinda, kwa hiyo nitoe ushauri kwa walimu wenzangu kwenye shule zingine, tujenge utamaduni wa kuwaleta  wanafunzi wetu Bungeni na maeneo mengine ili wajifunze,” alisema Mwalimu Joseph.

About The Author

error: Content is protected !!