
Mohamed Mchengerwa
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26 yenye takribani Sh. 11.783 trilioni kwa ajili ya wizara na taasisi zilizo chini yake. Anaripoti Apaikunda Mosha, Dodoma … (endelea).
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) leo tarehe 16 Aprili 2025 bajeti hiyo imeongezeka kutoka Sh. 10.125 trilioni zilizotengwa mwaka 2024/25 hadi kuwa na ongezeko la zaidi ya Sh. 1. 66 trilioni.
Mchengerwa amefafanua kuwa kati ya fedha hizo Sh. 3.95 trilioni zimeombwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo kati ya fedha hizo Sh 2. 5 trilioni ni fedha za ndani, ikijumuisha Sh 613.44 bilioni za mapato ya ndani ya halmashauri na Sh 1.45 trilioni ni fedha za nje.
Kwa upande mwingine amesema Sh 7. 84 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida yanayojumuisha mishahara Sh 6.3 trilioni na matumizi mengineyo Sh 1.53 trilioni ikijumuisha Sh 1.067 trilioni za mapato ya ndani ya halmashauri.
“Tumewasilisha si tu makadirio ya mapato na matumizi, bali tumeweka mbele yetu dira ya matumaini, ramani ya maendeleo na ahadi ya uongozi unaowajibika. TAMISEMI haitafuti sifa ya kisiasa, tunatafuta suluhisho sahihi kwa maisha ya mtanzania wa kawaida,”amesema Mchengerwa.
Aidha, Mchengerwa amesisitiza kuwa bajeti hiyo ni kwa ajili ya kuboresha maisha ya mtanzania wa kawaida hivyo ametoa wito kwa mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na wananchi wote kushirikiana ili kusonga mbele kwa mshikamano.
“Kwa dhamira hii, na kwa imani kubwa katika maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan tunawasilisha bajeti hii kama zana ya kazi, dira ya matumaini na silaha ya mapinduzi ya kiutawala, kiuchumi na kijamii.”
“Kwa hiyo, tunasema kwa ujasiri mkubwa, TAMISEMI, ndiyo msingi wa maendeleo endelevu. Kila Shilingi ina Jukumu, Kila Kiongozi ana Wajibu na Kila Mwananchi ana Nafasi!”
ZINAZOFANANA
Serikali yajivunia mafanikio sita ya TASAF
Dk. Kimei aweka rekodi ya utendaji Vunjo
Bashe atoa onyo kwa wasafirishaji wa bidhaa za kilimo Malawi na Afrika Kusini